Full-Width Version (true/false)


FULL STORI YA YULE MWANAUME KUOA MWANAUME MWENZAKE BILA KUJUA HUKO MTWARA

[​IMG] 
 Zamda

HII ni kali ya karne! Kijana Musra Nurdin Bicho (20) na Sharraf Issa Chimera (19) wameacha watu midomo wazi baada ya kufunga ndoa ya jinsi moja katika Kijiji cha Mpanyani mkoani Mtwara.

Tukio hilo lililovuta hisia za wengi, lilijiri hivi karibuni baada ya vijana hao kufunga ndoa ambayo katika mila na tamaduni za Kitanzania haikubaliki.


Kwa mujibu wa mashuhuda kutoka kijijini humo, Musra alifunga ndoa na mwanamke aliyemchumbia aliyemfahamu kwa jina la Zamda badala ya Sharraf, miezi sita iliyopita huku muoaji akiwa hajui kama anayemuoa ni mwanaume mwenzake.


ILIKUAJE?
Ilifahamika kuwa, Musra alianza uhusiano wa uchumba na Zamda. Uchumba huo ulidumu yapata miezi miwili huku kila mmoja akilinda ahadi ya kutokukutana kimwili hadi pale watakapokuwa wamefunga ndoa.


MWANAUME ASAKA MAHARI
Ilielezwa kwamba, baada ya kukubaliana kufunga ndoa, mwanaume muoaji (Musra) alifanya kazi ya kulima vibarua ili kupata mahari ya kumtolea mchumba wake huyo, jambo ambalo alifanikiwa.
KWA NINI HAKUJUA
Ilidaiwa kwamba, Zamda alipokutana na Musra alikuwa kwenye muonekano wa kike kuanzia kichwani hadi miguuni. Zamda alikuwa anasuka, anapaka wanja, rangi mdomoni, anajifunga mtandio, tembea na hata ongea yake ilimfanya Musra na watu wengine washindwe kushtukia kama si mwanamke.


WATAMBULISHANA KWA WAZAZI
Baada ya kuridhiana, Musra aliamua kumpeleka Zamda kwao na kutambulishwa kwa ajili ya ndoa.


WAZAZI WAKATAA KUBARIKI NDOA
Kwa mujibu wa mama wa Musra, Zainabu Ismail, alimuuliza muoelewaji kama amekubaliwa na wazazi wake, akasema ndiyo, lakini kila alipoambiwa awape namba za simu za wazazi wake ili wajiridhishe hakukubali.
Baada ya kuona hivyo, wazazi wa Musra walikataa kubariki ndoa hiyo.


‘MWANAMKE’ ANG’ANG’ANIA NDOA
Ilisemekana kwamba, Zamda alipoona wazazi wa Musra hawataki wafunge ndoa, alishauriana na mwanaume kuwa wafunge hivyohivyo.


WATINGA KWA SHEHE
Ilielezwa kwamba, katikati ya sintofahamu hiyo, wawili hao walikubaliana kisha wakamtafuta shehe aliyetajwa kwa jina moja la Hidary ambaye naye aliwauliza kama wana baraka za wazazi wa pande mbili, wakachengachenga, lakini mwisho shehe huyo aliwafungisha ndoa.


SIKU SABA BILA UNYUMBA
Ilisemekana kwamba, ndoa hiyo ilipokamilika, wapenzi hao walianza maisha ya ndoa ya mke na mume, lakini kila siku mwanaume alipokuwa akiulizia unyumba, hakupewa kwa madai kuwa, mwanamke alikuwa ametoka kupewa mimba muda si mrefu na ana matatizo asubiri apone (bila kufafanua kivipi).


MASHTAKA KWA MAMA
Habari zilieleza kuwa, Musra aliamua kwenda kwa mama yake kwa ajili ya kushitaki ambapo mama yake alimuomba amvumilie mwenzake pengine kweli alikuwa anaumwa.


SIKU ZAONGEZEKA BILA UNYUMBA
Ilidaiwa kwamba, tendo la kunyimwa unyumba liliendelea hadi wiki ya pili, mwanaume akaamua kwenda tena kwa mama yake na kuuliza mwanamke anayekuwa kwenye hedhi huwa anamaliza baada ya siku ngapi maana zilikuwa zimekatika wiki mbili.

Alijibiwa kuwa, itakuwa si hedhi labda atakuwa na chango tumboni.


MIEZI MITATU
Mashuhuda walisema kuwa, Musra aliendelea kuvumilia hadi miezi mitatu bila kukutana kimwili na ‘mkewe’ huyo kwa madai kuwa anaumwa. Baadaye mwanaume aliamua kumuacha, lakini haukupita muda, walirudiana.


ASHIRIKIANA NA WANAWAKE
Akizungumza na Wikienda, mmoja wa wanawake ambao walikuwa wakishirikiana na ‘mwenzao’ bila kujua ni mwanaume, alisema:

“Tulikuwa tunashirikiana naye kwenye mambo ya wanawake, kama kucheza rede, kwenda kukata kuni, kuosha vyombo, kufua na kazi nyinginezo. Kuna wakati mumewe akiwa hayupo tulikuwa tunampa wasichana anaenda kulala nao kwake.”


KAZI ZA KIKE YUKO FASTA
Ilisemekana kwamba, kitu kingine kilichofanya ashindwe kushtukiwa mapema ni kitendo cha kuonekana yuko fasta na vizuri katika kufanya kazi zote za kike kama mwanamke halisi.


VIPI KUHUSU MATITI?
Ilielezwa kwamba, kimaumbile alionekana mwanamke kwa sababu alikuwa ametengeneza matiti feki kwa kuweka sponchi na kuyabana vizuri kwa sidiria.


KUBAINIKA KWAKE SASA
Ilidaiwa kuwa, ndugu zake ‘mwanamke’ walikwenda katika kijiji hicho cha jirani kwa ajili ya kumtafuta ndugu yao wakiwa na picha. Walipowaonesha wenyeji wakaonekana kumfahamu kuwa ni mke wa Musra, ndugu wakashangaa mbona ndugu yao ni mwanaume?


MWANAMKE FEKI ASEPA KIAINA
Baada ya kuona mchongo umebumburuka, Zamda aliamua kusepa kiaina, lakini hakufika mbali, akawa ametiwa mikononi mwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpanyani, Mohamed Mtota.


KWA MWENYEKITI
“Hili tukio ni la kushangaza sana kwani siku zote hata mimi najua huyo mtu ni mwanamke kutokana na muonekano na matendo yake. Nilipopokea mashitaka kuwa ni mwanaume, nilishangaa, nilimuingiza kwenye chumba akafanyiwa upekuzi na kubaini kweli ni mwanaume.


WANANCHI WALITAKA KUMUUA
“Baada ya wananchi kuona kuwa ni kweli mwanaume wakataka kumpiga na kumuua, ikabidi nipige simu kituo cha polisi ndipo wakaja wakachukuliwa na kupelekwa kituoni,” alisema mwenyekiti huyo alipozungumza na Wikienda.


SHEHE ATOWEKA, ASAKWA
Hata hivyo, kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, jeshi la polisi linaendelea kumsaka Shehe Hidary ambaye alifungisha ndoa hiyo huku wahusika hao nao wakiwa wanashikiliwa na polisi.


STORI: GABRIEL NG’OSHA | IJUMAA WIKIENDA |MTWARA

No comments

Powered by Blogger.