Full-Width Version (true/false)


Bajeti finyu yamkwaza CAG


MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, amesema Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti unaosababisha shughuli za kiofisi kutofanyika.

Aidha, amesema hali hiyo pia inakwaza  utekelezaji wa majukumu ya dharura yanayoibuka nje ya ukomo wao wa bajeti.

Kadhalika,  amesema ofisi yake imefanikiwa kufanya kaguzi za Umoja wa Mataifa kwa ufanisi tangu walipolipokea jukumu hilo kutoka Ofisi ya SAI-China hadi watakapoikabidhi kwa Chile mwezi ujao.

Prof. Assad alieleza hayo jana jijini hapa kwenye mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, wenye lengo la kupitisha bajeti ya mwaka na kujadili masuala ya kiutendaji ambayo yanawasilishwa na kuitishwa na wajumbe.

“Baraza hili limekuwa na ufanisi mkubwa katika kusimamia majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye mkataba,” alisema Prof. Assad

Alisema pamoja na mafanikio ambayo ofisi hiyo imeyapata, bado zipo changamoto zinazoikabili na zinahitaji utatuzi.

Alizitaja changamoto nyingine ni kushindwa kukamilisha ujenzi kwa ajili ya ofisi katika mikoa iliyolengwa kutokana na kutotolewa kwa wakati  kwa fedha za maendeleo kama ilivyopangwa.

“Ukosefu wa vitendea kazi muhimu kwa ajili ya watumishi ikiwamo magari kwa ajili ya usafiri na kompyuta mpakato kwa ajili ya uandaaji wa ripoti ya ukaguzi, hii ni changamoto nyingine,” alisema CAG.

Alibainisha katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa Fedha 2017/18 hadi kufikia Machi, 2018 ofisi ilishindwa kuwajengea uwezo watumishi kulingana na viwango vya kimataifa vya ukaguzi kutokana na ufinyu wa bajeti.

“Kuna changamoto ya mwenendo wa upatikanaji wa fedha za matumizi mengineyo na maendeleo kutoka mfuko mkuu wa serikali kutoendana na mahitaji halisi ya majukumu ya taasisi hususani ukaguzi na mafunzo kwa watumishi,” alisema.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana alisema ofisi yake imefanikiwa katika kutoa taarifa kwa wakati, kila ilipofika Machi 30, kila mwaka.

“Pia tuliweza kutekeleza majukumu yetu kwa kutoa mapendekezo ya ukaguzi kwa kuzingatia dira ya serikali ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda,” alibainisha.

Prof. Assad aliiomba ofisi ya Katibu Mkuu Utumishi iwasaidie kutatua changamoto zinazowakabili ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Dk. Laurean Ndumbaro, aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, aliitaka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kutekeleza agizo la serikali kuhamishia shughuli zake mkoani Dodoma.

Dk. Ndumbaro alisema viongozi na watumishi mbalimbali wa serikali walishahamia, hivyo ni mategemeo yake kuwa ofisi hiyo nayo pia ipo katika mkakati wa kuhamishia shughuli zake Dodoma kama ambavyo taasisi nyingine zimefanya.

No comments

Powered by Blogger.