Full-Width Version (true/false)


Bocco ahofia mechi yao ya leo

SIMBA imebakiwa na mechi mbili kwenye ligi kuu na kama hawatafungwa basi wataweka rekodi lakini mshambuliaji wao hatari, John Bocco ameingiwa na hofu kuwa huenda wakakamiwa ili wasifikie malengo.

Simba tayari ni mabingwa wa ligi kuu msimu huu na mpaka sasa hawajapoteza mchezo wowote kati ya 28 waliyocheza na wamebakia na mechi dhidi ya Kagera Sugar leo Jumamosi na Majimaji utakaopigwa Mei 28, mwaka huu kule Songea, Ruvuma.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Bocco alisema mechi hizo zitakuwa na ugumu kutokana na rekodi yao nzuri ya kutopoteza mechi zilizopita, hivyo wapinzani wao wanaweza wakawapania ili wavunje rekodi wanayokaribia kujiwekea lakini wao watakaza kuhakikisha mambo hayaharibiki.

“Sisi tayari tumechukua ubingwa lakini mechi zetu mbili zilizobaki zitakuwa ngumu kwa kuwa watataka kutuharibia rekodi ya kuchukua ubingwa bila kufungwa.

“Hata hivyo tumejipanga kuhakikisha tunashinda michezo yote ili kuweka rekodi ya kuchukua ubingwa bila kufungwa,” alisema Bocco.
Bocco tayari amefunga mabao 14 kwenye ligi huku Mganda, Emmanuel Okwi akiongoza akipachika 20 katika msimu huu.

No comments

Powered by Blogger.