Full-Width Version (true/false)


Bunge, CHADEMA wavutana mazishi ya Bilago
Wakati wananchi na viongozi wakiomboleza kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago kumekuwepo na mkanganyiko wa taarifa kutoka Ofisi ya Bunge na viongozi wa CHADEMA kuhusu siku rasmi ya mazishi ya Mbunge huyo. 
Katika ibada maalumu ya kuaga mwili wa Mbunge huyo iliyofanyika leo Mei 28, 2018 katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe amesisitiza kuwa siku ya mazishi ya mbunge ni Alhamisi Mei 31, 2018.

“Siku ya Alhamisi tutampeleka kanisani kwa ibada maalumu kwajili ya maziko yake, kisha tutakwenda kwenye shamba la familia kwaajili ya kumlaza, lakini Bunge bado linasisitiza tutamzika Jumatano, mimi namwambia Spika (Job Ndugai) na timu yake watazika mtu wao wanayemtaka, Mbunge wetu tutamlaza siku ya Alhamisi” amesema Mbowe.

 Mwenekiti huyo ameongeza kuwa kama Bunge halitaonesha ushirikiano na viongozi wa chama hicho pamoja na familia basi kama viongozi wa chama watakuwa tayari kugharamia kila kitu pasipo msaada wa Ofisi ya Bunge.

Mapema leo Mei 28, 2018 Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson akitangaza kuaihirisha kikao cha Bunge Jijini Dodoma ili kuomboleza kifo cha mbunge huyo, Naibu spika aliweka wazi ratiba ya mazishi itakua ni Jumatano Mei 30, 2018 katika Kijiji cha kasuga wilaya Kakonko mkoani Kigoma.

Marehemu Kasuku Bilago alikuwa Mbunge wa jimbo la Buyungu kupitia CHADEMA alifariki Dunia Mei 26, 2018 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
 

No comments

Powered by Blogger.