Full-Width Version (true/false)


CHADEMA yatoa ratiba yake
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa rasmi ratiba ya kuuaga na kumzika marehemhu Kasuku Bilango aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma ambaye amefariki mwishoni mwa juma lililoisha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili akipatiwa matibabu. 

Ratiba hiyo imewekwa wazi na Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje ya CHADEMA, John Mrema na kusema baada ya kikao kilichokaliwa baina ya familia na viongozi wakuu wa chama hicho Mei 27, 2018 walikubaliana siku ya leo kufanyike ibada fupi na kuuaga mwili katika viwanja vya Karemjee Jijini Dar es Salaam majira ya saa sita mchana na mwishowe mwili huo kupelekwa uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya kupelekwa Bungeni Jijini Dodoma ili wabunge wapate kuuaga siku ya kesho katika viwanja vya Bunge.

Aidha, Mrema amesema baada ya zoezi hilo kukamilika kwa Wabunge mwili wa marehemu Kasuku utasafirishwa kwa ndege kuelekea Kibondo ambapo itakapofikia siku ya Jumatano Mei 30 wananchi wa Jimbo la Buyungu watapata fursa ya kuuga mwili katika eneo ambalo litatangazwa baadae.

"Mei 31 ndio siku ya mazishi rasmi ambayo yatafanyika nyumbani kwa marehemu huko Wilayani Kakonko, Kigoma. Tunatoa wito kwa wanachama, wapenzi na watanzania wote tuendelee kuikumbuka familia ya marehemu katika sala na dua katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao ili Mungu aendelee kuwapa faraja",imesema taarifa hiyo.

Enzi za uhai wake Mhe. Kasuku Bilango alikuwa Mbunge wa Jimbo la Buyungu, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Magharibi yenye Mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora. 

No comments

Powered by Blogger.