Full-Width Version (true/false)


Dada wa Masogange Naye Afunguka Sakata la Steve Nyerere Kutafuna Rambirambi

Siku moja baada ya msanii Steve Nyerere, kudaiwa kutafuna michango ya msiba wa video Qeen, Agnes Masogange, dada yake Emmy Gerald amesema msimamo wake hautofautiani na kamati ya mazishi inayosimamiwa na msanii huyo ya kumfungulia mtoto akaunti kama ilivyopangwa hapo awali.

Akizungumza na  MCL Digital leo Mei  11, Emmy amesema siku mbili hizi anatarajia kuwapa taarifa kamili za mtoto huyo ili waweze kumwekea hela yake kama ilivyopangwa.

“Jamani naomba watu wapuuze maneno yanayosemwa kuhusu hiyo michango, mimi naungana na kamati ya mazishi kumfungulia mtoto akaunti na nitawapa taarifa zake kamili kwa ajili kuanza mchakato wa kuifungua, kwani tayari nimeshapata ujumbe wao wa kulitaka hilo,” amesema dada huyo.

Hata hivyo, amesema kwa huyo aliyeenda kulalamika kwenye vyombo vya habari ni ndugu wa mwanaume aliyezaa na Masogange na kueleza jambo lolote linalohusu hayo aulizwe yeye kwa kuwa ndio msemaji wa familia upande wa kina Masogange.

Alipoulizwa kama wana mahusiano mazuri na upande wa baba wa mtoto, alisema hawana tatizo lolote na kueleza kwamba hivi karibuni wanatarajia kuwa na kikao cha wana ndugu kwa ajili ya kuzungumza mambo mbalimbali ikiwemo arobaini yake.

“Unajua haya mambo kwa sasa sitaki kuyaongea sana kwenye vyombo vya habari, kwani kuzungumza ni sawa na kumsengenya marehemu ambaye ana siku chache tangu tulivyompumzisha, nitaongea mengi siku ya arobaini ikiwemo kuwashukuru watu walivyoshiriki katika msiba wake hayo mambo mengine naomba watu wayapuuze,” amesema Emmy.

Jana mweka hazina wa kamati ya mazishi ya Masogange, Zamaradi Mketema alisema Sh2.1 milioni zilizobaki katika mazishi anazo yeye na anachosubiri ni kupata taarifa kamili za mtoto ili waweze kumfungulia akaunti hiyo.

Masongane alifariki Aprili 20, mwaka huu, akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Mama Ngoma, na kuzikwa Aprili 23 kijijini kwa baba yake Utengule Mbeya.

No comments

Powered by Blogger.