Full-Width Version (true/false)


FUNGA YA RAMADHAN:Mambo yanayobatilisha funga,sehemu ya1
KULA NA KUNYWA:-
Ikiwa mtu mwenye funga atakula au atakunywa kitu kwa makusudi, basi funga ya mtu huyo itakua ni yenye kubatilika, iwe kula huko kula ni kula chakula au kula kitu chengine kama vile udongo au utonvu wa mti, kiwe kitu hicho ni kidogo au kingi, hata uzi ikiwa mtu atautia mdomoni kisha akautoa nje halafu akautia tena mdomoni kisha akameza ule umaji maji uliokuwemo kwenye uzi huo, funga yake itabatilika, na vile vile umaji maji wa msuaki unabatilisha saumu ikiwa ataumeza, isipokua umaji maji huo ukiwa utapokua umetoweka ndani ya mate kiasi cha kua hauitwi tena kua ni umaji maji wa msuwaki bali unahesabika ni kama mate tu, na chakula kilichoganda kwenye meno kinabatilisha saumu ikiwa mtu atakimeza.

Ikiwa mwenye saumu atakunywa au atakula kitu kwa kusahau, mtu huyo haitobatilika funga yake.

Mwenye saumu anatakiwa kujiepusha na kupiga sindano zinazotumika badala ya chakula , lakini hakuna tatizo kupiga sindano za ganzi au sindano za dawa yaani sindano zisizokua na chakula ndani yake.

Ikiwa mtu atakua anakula usiku kisha akafahamu kua imeshaingia Asubuhi, basi anatakiwa kuitema ile tonge iliokuwemo mdomoni mwake, na akiimeza kwa makusudi tonge hiyo, basi funga yake itabatilika, na mtu huyo atawajibika kulipa kafara, kama vile tutavyokuja kulizungumzia suala hilo baadae.

Ikiwa mwenye funga atakua na kiu kali kiasi cha kuhatarisha maisha yake, mtu huyo anaruhusiwa kunywa maji kwa kiasi cha kuyaokoa maisha yake, lakini funga yake itabatilika, na ikiwa funga aliyokua nayo ni funga ya Ramadhani, basi hotoruhusiwa mtu huyo baada ya kunywa maji hyo kutenda matendo yenye kubatilisha saumu, na vile vile atatakiwa kuilipa funga hiyo.

Si wajibu kwa mtu mwenye kufunga kusafisha meno yake kabla ya adhana ya Asubuhi, lakini akiwa atafahamu kua chakula kilichobakia menoni kitateremka tumboni baadae (wakati wa funga), na akawa hakuyasafisha meno yake, saumu ya mtu huyo itabatilika, kiwe chakula hicho kimeteremka au hakikuteremka, katika hali zote mbili saumu yake itabatillika.

Kuyameza mate yaliotunduwia mdomoni kwa kutokana na kufikiria (kutamani) kitu kikali kama vile embe mbichi, au mate hayo yaikusanyika bila ya kufikiria kitu,basi mate hayo si yenye kubatilisha saumu.

Hukubatilishi saumu kumeza makohoo ambayo bado hayajaingia kwenye uwanja wa kinywa (yaani yakiwa bado yapo kwenye uwanja wakoo), na vile mafua ambayo yanatoka kwenye tondu za pua za ndani ya mdomo, iwapo mafua hayo yatakua hayakufika kwenye uwanja wa mdomo bali yakateremkia kooni moja kwa moja, basi hakuna tatizo kuyameza, lakini ikiwa makohoo hayo au mafua hayo yatakuja kinywani, katika hali hii basi yanatakiwa kutemwa.

Kukichakua chakula kwa ajili ya mtoto au ndege na vile vile kuonja chumvi, ambapo kwa kawaida tendo hilo hilisababishi vitu hivyo kufika kooni, na mfano wa mambo kama hayo, mambo hayo hayabatilishi saumu hata kama itatokezea bahati mbaya kitu hicho kikafika kwenye koo, lakini ikiwa mtu tokea mwanzo atajua kua akifanya hivyo kitu hicho kitateremka kooni, na alipofanya kikaenda kooni, basi saumu yake itakua imebatilika, na atatakiwa kuilipa funga hiyo na vile vile atawajibika kutoa kafara.

 Mtu haruhusiwi kula kwa kutokana na kwamba yeye ni dhaifu, isipokua udhaifu wake ukiwa mkubwa kiasi ya kwamba yeye hawezi kuihimili saumu, katika hali kama hii mtu huyo ataruhusiwa kula.


 2.KUJAMII/Tendo la ndoa
Kujamii iwe ni kwa njia ya mbele au nyuma, awe ni mtoto au mtu mzima, funga za wote wawili hua ni zenye kubatilika muingiliaji na muingiliwaji, hata kama kikiingia kichwa cha dhakar tu na manii yakawa hayakutoka, funga zao ziabatilika.

Ikiwa mtu atasahau na akafanya kitendo cha kujamii au akafanya kitendo hicho hali akiwa usingizini, au akiwa amelazimishwa na akafanya kitendo hicho bila ya hiyari, funga ya mtu huyo haitobatilika, lakini alifanya akiwa usingizini, basi akizinduka huku akiwa katika hili hiyo, basi anatakiwa papo hapo aache kufanya hivyo, au akiwa amelazimishwa halafu akaachiliwa na kupewa uhuru, vile vile anatakiwa kuwacha kitendo hicho papo hapo bila ya kuchelewa, na akiwa hakuacha bali akaendelea kufanya, funga yake itabatilika.

Ikiwa mtu atatilia shaka kua je alipoingiza dhakar kilichoingia ndani ya utupu kimefikia kiwango cha kichwa au la? Funga yake itasihi, na vile vile mtu aliye katwa au aliyekua hana kichwa cha dhakar akiwa atatilia shaka kua je sehemu aliyoiingiza imefikia kiwango cha kichwa au haikufikia? Funga ya mtu huyo vile vile itakua ni sahihi.


KUPIGA PONYETO
Ikiwa mwenye kufunga atapiga ponyeto na manii yake yakatoka, basi funga yake itabatilika, lakini ikiwa mtu atatoka manii bila ya hiyari yake, funga yake haitobatilika, lakini ikaiwa atafanya jambo litalosababisha kutoka manii hayo bila ya hiyari, funga yake itabatilika.

Wakati wowote ule mwenye funga akifahamu ya kua akilala atajiotea (ataota ndoto itayomsababishia kutokwa na manii), hakuna tatizo mtu huyo kulala, na ikiwa atalala kisha akatokwa na manii, funga yake itasihi, khususan mtu huyo kama atakua kuto kulala, kwake yeye ni jambo zito ambalo laweza kumletea madhdra.

Mtu aliyetokwa na manii usingizini anaweza kukojoa kabla ya kuoga kisha akajikamua kama vile lilivyoelezewa jambo hilo katika sehemu yakelakini iwapo atakua ameshakoga, na akaelewa kua ikiwa atakojoa kisha akajikamua manii manii hayo yatatoka nje, basi mtu huyo hatakiwi kujikamua, na ikiwa mtu aliyefunga atatokwa na manii hali akiwa usingizini, kisha akasihtuka hali yakiwa manii hayo yanatoka, mtu huyo halazimiki kuyazuwiya manii hayo yasitoke.

Mtu aliyetokwa na manii usingizini ikiwa ataelewa ya kua manii yamebakia ndani ya utupu wake, kisha akawa hakukojoa kabla ya kukoga, basi ni bora mtu huyo akojowe kabla ya kukoga.

Ikiwa mtu atakusudia kujitoa manii (kupiga ponyeto) kisha manii hayo yakawa hayakutoka, funga yake haitobatilika.

Ikiwa mtu atataniana na mwenziwe bila ya kukusudia kujitoa manii lakini manii yake yakatoka, basi ikiwa mtu huyo atakua anajua ya kua ana kawaida ya kutokwa na ikiwa atafanya utani wa aina kama hiyo, basi funga yake itabatilika, lakini ikiwa hana kawaida ya kutokwa na manii kwa utani wa aina kama hiyo lakini imetokezea bahati mbaya tu akatokwa na manii, katika hali hii vile vile funga yake itabatilika, isipokua akiwa na yakini ya kua akifanya utani huo hatotokwa na manii.KUMZULIA UWONGO MUNGU NA MTU WAKE
Ikiwa mwenye funga atafanya kwa makusudi kumzulia uwongo Mungu na Mtume wake (s.a.w.w) au kuwazulia uwongo Maimamu (a.s) kwa kutumi njia moja wapo, iwe ni kwa ulimi, kuandika au kuashiria, hata kama baada yakumaliza tu akatubia au akasema kua nimesema uwongo, funga ya mtu huyo itabatilika, na vile vile kunabatilisha saumu kuwazulia uwongo mitume wengine pamoja na waliokamata nafasi zao baada yao, pamoja na Fatima (a.s).

Ikiwa mtu atataka kunukuu habari ambayo haitambui kua ni ya ukweli au ya uwongo, basi wakati wa kuinukuu hatakiwi kuikatia kauli kwa namna fulani habari hiyo, lakini ikiwa kwa namna fulani ataikatia kauli habari hiyo, funga yake haitobatilika, awe katika hali ya kuidhania uwongo habari hiyo au awe anaifikiria kua ni ya kweli.

Ikiwa mtu atalitaja jambo fulani huku akiwa na yakini kua linatokana na kauli ya Mwenye enzi Mungu au Mtume wake (s.a.w.w), halafu baadae akafahamu kua jambo hilo lilikua ni la uwongo, hatobatilika funga yake.

Ikiwa mtu atakua anaelewa ya kua kumzulia uwongo Mungu na Mtume wake (s.a.w.w) kunabatilisha saumu kisha akayachukua maneno ya uwongo na kuyanasibisha kwao, kisha baadae akaelewa kua yale maneno aliyoyanasibisha kwao yalikua ni ya kweli, funga ya mtu huyo itakua ni sahihi.

Ikiwa mtu atauchukua uwongo uliotungwa na mtu mwengine kisha akaunasibisha kwa Mungu na Mtume wake (s.a.w.w) au kwa Maimamu (a.s), funga yake itabatilika, lakini ikiwa ataunukuu kutoka kwa mtu aliyeutunga uwongo huo, funga yake haitobatilika.

Ikiwa mwenye kufunga ataulizwa kua je maneno haya amesemwa na Mtume (s.aw.w)? naye pahala ambapo anatakiwa kusema ndiyo akasema hapana, na pahali pa kusema hapana akasema ndiyo, funga yake itabatilika.

Ikiwa mwenye kufunga atanukuu maneno sahihi kutoka Mola wake au Mtu wake (s.a.w.w), kisha baadae akasema maneno niliyoyasema hayakua ya kweli, au usiku wa funga akasema uwongo kisha asubuhi yake akasema kua yale niliyoyasema jana yalikua ni ya kweli, funga yake itabatilika.KUINGIZA VUMBI LILILO ZITO KOO

Kuingiza vumbi lililo zito kooni kunabatilisha funga, vumbi hilo liwe linatokana na kitu cha halali, kama vile vumbi la unga wa ngano, au liwe linatokana na kitu ambacho ni haramu kuliwa, kama vile udongo.

Mwenye funga hatakiwi kuingiza kooni mvuke ulio mzito, wala moshi wa sigara wala kitu chochote kile kinachofanafana na vitu hivyo.

Ikiwa mtu hakujilinda na vitu hivyo (hakuvijali), kisha ima vumbi au mvuke au moshi na mfano wake, kimoja wapo kikaingia kooni, hali ya kua mwanzo alikua na yakini kua kitu hicho hakitofika kooni,basi katika hali kama hii funga yake itakua nai sahihi, au akiwa amesahau kua amefunga akawa hajajichunga navyo au akawa kalazimisha kukitia kooni kitu hicho, katika hali hii vile vile funga yake itakua ni sahihi.


KUKIZAMISHA KICHWA NDANI YA MAJI AU KUPIGA MBWIZI
 Ikiwa mfungaji kwa makusudi atakizamisha kichwa chake majini hata kama sehemu nyengine ya mwili wake itakua imebaki nje, funga yake itabatilika, lakini kama mwili wake wote utakua ndani ya maji isipokua baadhi ya sehemu ya kichwa chake ikawa imebaki nje, funga yake haitobatilika.

Ikiwa mwenye funga, hivi sasa atatumbukiza ndani ya maji nusu ya kichwa chake kisha kwa mara nyengine akaja kuitumbukiza ile nusu iliyobakia, mtu huyo haitobatilika funga yake.

Ikiwa mtu atakua ana shaka kua je kichwa chake kimeingia chote kabisa ndani ya maji au kulikua na sehemu fulani iliobakia nje? Katika hali kama hii funga yake itakua ni sahihi.

Ikiwa kichwa chote kitakua kimezama majini ikabakia nje sehemu fulani tu ya nwele ambayo hakuzama majini, funga yake itabatilika.

Anatakiwa mwenye funga kujiepusha na kutumbukiza (kuzamisha) kichwa chake ndani ya maji yaliokua ni madhafu hasa hasa maji ya mauwa kama vile arki ya mauwa, lakini hakuna tatizo kutumbukiza kichwa katika aina nyengine za maji maji kama vile mafuta ya nazi au petrol.

Ikiwa mwenye funga atatumbukia majini bila ya kutaka na kichwa chake chote kikazama majini, au akawa amesahau kua yumo ndani ya funga akakitumbukiza kichwa chake chote majini, funga yake haitokua ni yenye kubatilika.

Ikiwa mtu anatambua kua ni kawaida yake akichupa ndani ya maji kichwa chake hua kinazama kwenye maji, kisha kwa makusudi akachupa kwenye maji na kichwa chake kikazama ndani ya maji, funga yake itabatilika.

Ikiwa mwenye funga atasahau kua kafunga, kisha kicha chake akakizamisha majini, au kuna mtu aliyemkamata kichwa chake kisha akakizamisha majini, basi ikawa atakumbuka hali ya kua kichwa chake kimo majini au yule aliyemkamata akakiachia kichwa chake, basi papo hapo anatakiwa kukitoa kichwa chake kutoka majini, na akiwa hakukitoa funga yake itabatilika.

Ikiwa mtu atasahau kua kafunga akatia nia ya kukoga josho fulani, halafu akakizamisha kichwa chake majini kwa nia ya kukoga josho hilo, basi funga yake itakua ni sahihi.

Ikiwa mtu ataelewa kua yuko kwenye funga, kisha kwa makusudi kwa ajili ya kukoga josho fulani akakizamisha kichwa chake majini, hali ya kua mtu huyo anayo funga ya wajibu  iliyokua imeainishiwa wakati maalum kama vile funga ya Ramadhani, basi mtu huyo atatakiwa kukoga tena kwa mara ya pili, na vile vile atatakiwa kuilipa funga ya siku hiyo, na ikiwa mtu atakua yuko ndani ya funga ya Sunna au funga ya Wajibu iliokua haikuainishiwa (haikuwekewa) wakati maalum, kama vile funga ya Kafara (kwa sababu funga ya Kafara haina wakati maalam), basi josho lake litakua ni sahihi lakini funga yake itabatilika.

Ikiwa mtu kakizamisha kichwa chake majini kwa ajili ya kumuokoa mtu fulani aliyekua akizama, ingawaje kumuokoa mtu huyo ni Wajibu lakini funga yake itabatilika.KUBAKI NA JANANABA, HEDHI AU NIFA HADI WAKATI WA ADHANA YA ASUBUGHI
Mtu mwenye kutaka kufunga Ramadhani au kuilipa funga ya Ramadhani, hatakiwi kubakia na janaba mpaka wakati wa adhana ya Asubuhi kwa makusudi, kwa hiyo basi akiwa mtu ataacha kukoga kwa makusudi, au katika hali ya dhiki ya wakati akawa hakutayammam, funga ya mtu huyo itabatilika.
Hakuna tatizo kubaki na janaba katika funga nyengine zisizokua za Ramadhani, funga hizo ziwe ni za Wajibu au Sunna.

Ikiwa mtu mwenye kufunga funga ya Ramadhani au mwenye kuilipa funga ya Ramadhani, hatokogo janaba mpaka ikafikia wakati wa adhana ya Asubuhi wala hakutayammam, lakini hakufanya hivyo kwa makusudi, bali labda alizuwiliwa na mtu fulani, basi funga yake itakua ni sahihi.

Mtu mwenye janaba ambaye anataka kufunga Ramadhani au kuilipa funga ya Ramadhani, ikiwa mtu huyo ataacha kukoga  kwa makusudi mpaka wakati ukawa ni mdogo kwa ajili ya kukoga, basi mtu huyo anaweza kufunga kwa kutayammam, na funga yake itakua ni sahihi.

Ikiwa mtu mwenye funga ya Ramadhani atasahau kukoga janaba, kisha baada ya kupita siku moja au kutapi masiku fulani akakumbuka, mtu huyo atatakiwa kuzilipa funga za masiku yote yale aliyofunga bila ya kukoga, na ikiwa atakuja kukumbuka baada ya kupita masiku, basi atatakiwa kuzilipa funga hizo kwa kadri ya yakini yake, yaani akiwa na yakini kua zilikua ni siku kumi ndizo alizobakia na janaba basi atatakiwa kuzilipa siku kumi, kwa mfano akiwa haelewi kua je zilikua ni siku tatu au nne? Basi atatakiwa kuzilipa siku tatu.
      
Ikiwa mtu mwenye funga ya Ramadhani atakua anaelewa kua hakuna wa kutosha kwa ajili ya kukoga wala kwa ajili ya kutayammam, basi mtu huyo akijisababishia kupata janaba kisha akapata janaba, funga yake itabatilika, na atawajibika kulipa funga ya siku hiyo pamoja na Kafara, lakini mtu huyo akawa anao wakati wa kuyammam kisha akajitia janaba halafu akatayammam, funga yake itakua ni sahihi, na hatohisabika kua kafanya kosa.

Mtu akiwa na janaba katika usiku wa mwezi wa Ramadhani, kisha akaelewa kua iwapo atalala basi hatoamka mpaka Asubuhi, mtu huyo basi hatakiwi kulala, na iwapo atalala na akawa hakuamka mpaka Asubuhi, basi funga ya mtu huyo itabatilika, na atawajibika kulipa funga pamoja na Kafara.

Wakati wowote ule wa usiku wa mwezi wa Ramadhani ikiwa mwenye janaba atalala kisha akaamka, na akawa anetegemea kua akilala tena  kwa mara ya pili ataamka ili aoge, basi anaweza kulala tena, iwapo itakua ni kawaida yake akilala kwa mara ya pili huamka.

Mtu mwenye janaba katika usiku wa mwezi wa Ramadhani, kisha akaelewa au akategemea kua akilala ataamka kabla ya adhana ya Asubuhi, na akawa ana nia ya kua akiamka atakoga, na akwa amelala huku akiwa na nia hiyo, lakini ikatokea bahati mbaya akawa hakuamka mpaka ukafika wakati wa adhana ya Asubuhi, funga ya mtu huyo itakua ni sahihi.   

Ikiwa mtu mwenye janaba katika usiku wa mwezi wa Ramadhani atafahamu au akatarajia kua ataamka kabla ya adhana, lakini akawa ameghafilika kua wakati atakaoamka anatakiwa kuoga, basi iwapo mtu huyo atalala na akawa hakuamka mpaka ukafikia wakati wa adhana ya Asubuhi, funga yake itakua ni sahihi.

Ikiwa mtu mwenye janaba katika usiku wa mwezi wa Ramadhani ataelewa au atatarajia kua akilala ataamka kabla ya adhana ya Asubuhi, basi ikiwa mtu huyo ameamua kua akiamka asioge, au akawa anatia akitoa kua hivi nikamka nioge au nisioge? Basi akilala katika hali kama hiyo kisha akawa hakuamka mpaka ukafika wakati wa adhana ya Asubuhi, funga yake itabatilika.

Ikiwa mtu mwenye janaba katika usiku wa mwezi wa Ramadhani, atalala kisha ataamka tena na akaelewa au akatarajia kua akilala tena ataamka kabla ya adhana ya Asubuhi, na akawa na nia kua akiamka ataoga, basi iwapo mtu huyo atalala tena kisha akawa hakuamka mpaka wakati wa adhana ya Asubuhi, mtu huyo atatakiwa kuilipa funga hiyo, na vile vile iwapo mtu huyo ataamka kisha akalala tena kwa mara ya tatu, lakini katika hali hii (yaani hali ya kua aliamka kisha akalala tena kwa mara ya tatu), atalazimika kuilipa funga hiyo pamoja na Kafara.

Usingizi ambao mtu amelala kisha akajiotea (akaota ndoto iliomsababishia kupata janaba) sio kwamba usingizi huo ndio huhisabiwa kua usingizi wa kwanza, bali iwapo ataamka katika usingizi huo hapo ndipo utakahisabiwa kua usingizi wa kwanza.

Iwapo mtu mwenye tapata janaba kwa njia ya ndoto katika nyakati ya mchana, basi hakuna ulazima juu yake kuoga papo hapo.

Wakati wowote ule katika mwezi wa Ramadhani iwapo mtu ataamka baada ya adhana ya Asubuhi kisha akajigutukia kua anajanaba lililosababishwa na ndoto, hata kama atelewa kua ndoto hiyo aliiota kabla ya adhana ya Asubuhi, funga yake itakua ni sahihi.

Mtu ambae anataka kulipa funga ya mwezi wa Ramadhani wakati wowote akija kubakia na janaba mpaka wakati wa adhana ya Asubuhi, hata kama atakua hakufanya kwa makusudi, funga yake itabatilika.

Mtu ambae anataka kulipa funga ya mwezi wa Ramadhani, akaamka baada ya adhana ya Asubuhi, kisha akaelewa kua ana janaba linalotokana na ndoto, na akaelewa kua aliota ndoto hiyo kabla ya adhana ya Asubuhi, basi ikiwa hana muda tena wa kuzilipa funga hizo, yaani kwa mfano anadaiwa funga za siku tano na zmebakia siku tano tu mpaka kuufikia mwezi mwezi mwengine wa Ramadhani, basi atatakiwa kufunga katika siku hiyo, kisha ukimaliza mwezi wa Ramadhani ailipe siku hiyo kwa mara ya pili, lakini ikiwa hana kizuizi kama hicho basi hatakiwi kufunga katika siku hiyo bali ailipe siku nyengine.

Ikiwa mtu katika mchana wa mwezi wa Ramadhani atakua na janaba lililosababishwa na ndoto, basi mtu huyo anaweza kufanya istibraa[5] kabla ya kukoga janaba, lakini iwapo atakoga janaba na baada ya kukoga akafahamu kua iwapo atafanya istibraa manii yatatoka nje, basi hatakiwi kufanya istibraa katika wakati huo.

Ikiwa mtu atafunga funga ya Sunna au funga ya Wajibu iliokua si miongoni mwa funga ya Ramadhani wala si funga ya kulipa deni la funga ya Ramadhani, kisha akabakia na janaba mpaka iakafika adhana ya Asubuhi, awe anajua ni wakati gani amepatwa na janaba au hajui, funga yake itakua ni sahihi.

Ikiwa mwanamke kabla ya adhana ya Asubuhi atasafika kutokana na damu ya hedhi au nifasi, kisha kwa makusudi akawa hakukoga, au ilikua wadhifa wake ni kutayammam na kwa makusudi akawa hakutayammam, haitosihi funga yake katika siku hiyo ikiwa funga hiyo ni ya Ramadhani au ni kwa ajili ya kulipa funga ya Ramadhani, bali katika funga nyengine zisizokua za Ramadhani vile vile anatakiwa kuyachunga mambo hayo.

Ikiwa mwanamke kabla ya adhana ya Asubuhi atasafika kutokana na damu ya hedhi au nifasi na akawa hana muda wa kukoga (yaani muda aliokua nao hadi kufikia wakati wa adhana hautoshi kwa ajili ya kukoga), iwapo mwanamke huyo atakua anataka kufunga funga ya Ramadahani, atayammam na funga yake itakua ni sahihi.

Ikiwa mwanamke baada ya adhana ya Asubuhi atasafika kutokana na damu ya hedhi au nifasi, au katika nyakati za mchana akatokwa na damu damu ya hedhi au nifasi, basi hata kama kitendo hicho kitakua kimetokea karibu na Maghari, katika hali zote hizo, funga yake itabatilika.

Ikiwa mwanamke atasahau kukoga josho la hedhi au nifasi, na baada ya siku moja au baada ya siku zaidi ya moja akakumbuka, basi funga zake alizozifunga katika kipindi hicho ambacho alikua amesahau kua hajakoga zitakua ni sahihi, lakini ili awe ametimiza wajibu wake ipaswavyo, ni vizuri kuzilipa funga hizo.

Ikiwa mwanamke kabla ya adhana ya Asubuhi atasafika kutokana na hedhi au nifasi kisha akafanya uzembe katika suala la kukoga, mpaka wakati wa adhana ukafika hali akiwa bado hajakoga, au kutokana na dhiki ya wakati vile vile akawa hakutayammam, basi funga yake ikiwa ni ya Ramadhani itabatilika, lakini ikiwa hakufanya uzembe katika kukoga, bali alikua akiwasubiri wanaume wamalize kuoga kwani hana sehemu nyengine ya kukogea isipokua hiyo, basi katika hali kama hii, hata kama atakua amelala kwa mara tatu, yaani analala akiamka huku akisubiri watu watoke chooni mwishowe ikafika Asubuhi hali akiwa hajaoga, funga yake itakua ni sahihi.

Ikiwa mwanamke atakua katika hali ya istihadha, na akakoga majosho yake kama inavyotakiwa, kama vile lilivyofafanuliwa suala hili katika mlango wa hukumu za mwanamke mwenye istihadha, funga ya mwanamke huyo itakua ni sahihi.

Mtu aliye gusa mwili wa maiti (yaani mwili wake ukagusana na mwili wa maiti bila ya kuwepo kizuizi), mtu huyo anaweza kufunga bila ya kukoga josho la maiti, na hata kama atafanya hivyo hali akiwa katika funga, funga yake haitobatilika.

Kutumia vitu vya aina ya maji maji kwenye njia ya siri hata kama itakua ni kwa ajili ya matibabu, hubatilisha funga, lakini iwapo vitu hivyo si maji maji, hakuna tatizo kutumia lakini ni vizuri kuto tumia vitu hivyo, kutumia vitu ambavyo havieleweki kua ni maji maji si maji maji, anatakiwa mtu kujiepusha navyo. 

ITAENDELEA........

No comments

Powered by Blogger.