Full-Width Version (true/false)


Imefahaamika,Ngassa amesaini mkataba wa miaka miwili Yanga

 

WINGA wa zamani wa Yanga, Mrisho Ngassa, amesaini mkataba wa miaka miwili wa kukitumikia kikosi hicho, akitokea Ndanda FC ya Mtwara.Imeelezwa kuwa mchezaji huyo ataanza kufanya yake ndani ya Yanga katika michuano ya SportPesa Super Cup inayotarajiwa kuanza wikiendi hii mjini Kisumu, Kenya. 

Ngassa alifika katika makao makuu ya Yanga yaliyopo makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam jana tayari kwa kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika na Katibu Mkuu, Charles Mkwasa. 

Mara baada ya kuwasili katika eneo hilo, mashabiki wa Yanga waliokuwapo nje ya jengo lao, walisikika wakimshangilia mno wakisema; ‘uncle (mjomba) karibu nyumbani’, huku akitabasamu na kuwapungia mikono kuonyesha kufurahishwa kwa kitendo hicho dhidi yake. Ngassa amekuwa katika rada za Yanga kwa muda mrefu, lakini kilichokuwa kinazuia usajili wake ni madai ya Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga ambaye alidaiwa kutotaka winga huyo kurejea Jangwani. 

Lakini ikumbukwe kuwa Sanga amerejea Yanga, ikiwa ni siku moja baada ya BINGWA kuripoti habari ya Sanga kuweka wazi kutokuwa na kinyongo na mchezaji wao huyo aliyewatumikia kwa mafanikio makubwa. 

Akizungumza na BINGWA katika ofisi za Yanga jana, Ngassa ambaye mkataba wake na Ndanda umemalizika, alisema amefurahi mno kurejea katika timu hiyo akiahidi kuipa mafanikio makubwa msimu ujao, akianzia na michuano ya SportPesa nchini Kenya iwapo atapewa nafasi. 

“Mimi sina neno na Yanga, ninaifahamu na ninajua mashabiki wanahitaji nini kwa sasa, nitatumia uzoefu wangu kuifanya Yanga iwe na mafanikio msimu ujao,” alisema Ngassa. Kwa upande wake, mshambuliaji wa kikosi hicho, Amissi Tambwe, aliunga mkono ujio wa Ngassa akielezea kufurahishwa kwake kwa kitendo hicho akiamini winga huyo atakuwa ni msaada mkubwa kwao. 

“Ngassa ni mchezaji mzuri, huwezi kumfananisha na wachezaji wengine waliopo, lakini pia ana uzoefu wa michuano ya kimataifa na anaifahamu vizuri ligi ya Tanzania,” alisema Tambwe. Kwa mara ya mwisho, Ngassa aliichezea Yanga msimu wa 2014/15 kabla ya kutimkia Free State Stars ya Afrika Kusini. 

source: BINGWA

No comments

Powered by Blogger.