Full-Width Version (true/false)


Kipa wa Liverpool Loris Karius ashauriwa ahame

 
Mlinda lango wa Liverpool Loris Karius ameshauriwa ahamie taifa jingine kucheza soka baada ya makosa mawili kuchangia klabu hiyo kufungwa magoli mawili katika fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Jumamosi.
 

Mjerumani huyo mwenye miaka 24 analaumiwa kwa kuwasaidia Real Madrid kushinda 3-1 kwenye fainali hiyo iliyochezewa mjini Kiev, Ukraine.
 

Karius alitokwa na machozi baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa huku akionekana mwenye masikitiko makubwa.
 

Baadaye aliwaomba radhi wachezaji wenzake, wakufunzi na mashabiki.
 

Kipa wa zamani wa England Robert Green ambaye mwenyewe aliwahi kufanya makosa kama hayo anasema: "Iwapo atarudi Ujerumani, ni kweli watu hawawezi kusahau alichokifanya lakini hataangaziwa zaidi."
 

"Kutoangaziwa sana kunaweza kuwa jambo zuri, kwenye ligi ya nyumbani, kwenda nje ya nchi ambapo watu hawakuwa wanajishughulisha sana na mechi hiyo."

Kosa la Green wakati wa Kombe la Dunia mwaka 2010 lilimfanya kufungwa bao rahisi na kusababisha mechi yao dhidi ya Marekani kumalizika 1-1.

Anasema tukio kama hilo linaweza kuwa ngumu sana kwa mlinda lango yeyote yule.

"nakumbuka baada ya Kombe la Dunia 2010 na mechi yangu ya kwanza ugenini Ligi ya Premia, kila nilipougusa mpira kulikuwa na watu kama 30,000 hivi uwanjani walikuwa wanapiga mbinja," anasema Green ambaye alichezea Norwich, West Ham, QPR na Leeds.

"Bahati mbaya kwa Karius ni kwamba nusu ya mechi ligini Uingereza ni za ugenini na anapokuwa upande wa mashabiki wageni hata uwanja wa Liverpool atakuwa anachekwa hata zaidi kama ugenini. Kipindi hiki cha kabla ya msimu kitakuwa kigumu sana kwake bila shaka.

"Makosa hutokea wakati wowote, yanaangazia zaidi unapokuwa mlinda lango ... lakini ukweli ni kwamba makosa yake yaliwagharimu ushindi mechi hiyo. Hilo litamkwamilia kwa muda lakini muhimu ni jinsi atakavyolipokea na natumai kwamba yeye kama binadamu na kipa ataweza kujikwamua na kurudi akiwa imara zaidi.

Mjerumani huyo alimpa mshambuliaji wa Real Madrid Karim Benzema bao rahisi la kwanza mjini Kiev.

Baadaye, alimruhusu Gareth Bale kufunga bao la tatu la Real kutoka mbali alipojaribu kuzuia kombora lake lakini likapita mikono yake na kutumbukia wavuni.

Hilo liliwawezesha Real kushinda taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya tatu mtawalia.

No comments

Powered by Blogger.