Kocha wa Ndanda aapa kufa na Simba Jumapili

KOCHA wa timu ya Ndanda FC Malale Hamsini amesema wapo tayari kufia
uwanjani kwenye pambano lao la Ligi Kuu Jumapili hii dhidi ya Simba SC
ili wapate japo pointi moja itakayowasaidia kwenye harakati za kujaribu
kujitoa kwenye janga la kushuka daraja.
Wakati kocha huyo akipanga hayo hajaacha kukiri ugumu atakaokumbana
nao kwenye mpango wake kutokana na Simba kuukaribia ubingwa huku pia
wakicheza kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Malale
amesema hakuna asiyejua kwamba Simba ni timu nzuri ndio maana wanaongoza
ligi tena kwa pointi nyingi lakini watapambana wapate hata sare katika
mchezo huo.
“Ukweli hakuna asiyejua kwamba Simba wanatisha, tunaenda kucheza nao tukijua kwamba wanatafuta pointi tatu ili wazidi kuusogelea ubingwa lakini na sisi tupo kwenye hatari ya kushuka daraja hivyo tutaenda kujitoa muhanga hata tufie uwanjani ilimradi tusitoke bila pointi,” alisema Malale.
Kwa upande mwingine Malale amesema timu yao itaondoka Mtwara jioni
ya leo kuja Dar es salaam bila ya kiungo wao mahiri Jabir Azizi
atakayeukosa mchezo huo kwasababu ana kadi tatu za njano.
Wakati Ndanda wenye michezo 26 wakipambana kujinasua kwenye janga la
kushuka daraja wakiwa katika nafasi ya 15 na pointi zao 23, Wekundu wa
Msimbazi wao wanatafuta pointi tano tu ili waweze kutwaa ubingwa wa
msimu huu.
No comments