Full-Width Version (true/false)


Mashabiki Arusha waitaka Yanga Kombe la ubingwa lirudi mwakani


Arusha . Ligi kuu Tanzania Bara imefikia tamati huku waliokuwa mabingwa watetezi Yanga wakimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kuchapwa jumla ya mabao matatu na timu ya Azam waliokuwa wanawania kwa pamoja angalau nafasi ya pili.
Yanga imemaliza msimu huu kwa kushika nafasi ya tatu badala ya kutetea ubingwa  kutokana na Wekundu wa Msimbazi Simba kunyakua kombe hilo kabla ya mechi tatu za kuhitimisha ligi.
Hata hivyo katika mchuano huo wa mwisho wa kumaliza ligi, wanachama wa Yanga Arusha wamefunguka kuwa kiwango walichocheza kikosi chao si cha kawaida wala kuzidiwa bali ni kama kuna mgomo baridi kati yao.
Mmoja wa wanachama hao Arusha, Rashidi Nchimbi alisema kuwa kikosi cha Yanga dhidi ya Azam waliingia uwanjani wakiwa na kama mgomo kwani hawakuwa na ari na mchezo na hata uwanjani hawakuonyesha kiwango walichokizoea.
“Uwezo waliokuwa wanatuonyesha wachezaji wetu mechi za awali ni tofauti  kabisa na jinsi kwa sasa hizi mechi za mwisho wanavyocheza tangu tu hali ya sintofahamu ya uchumi wa Yanga kuyumba. Mfano mzuri kikosi hichi cha jana ndio kikosi kilichocheza mechi ya kwanza na Azam na walishinda iweje hii wapoteze.”
“Kama umetazama mechi ya vizuri, utakuwa shahidi wangu baadhi ya wachezaji kama  Obrey Chirwa, Shishimbi (Papy) na wengine ni kama wana mgomo fulani hivi. Wanacheza kama wamepoteana kitu ambacho kwa mwaka huu kiukweli acha tu ligi iishe tujipange vizuri msimu ujao maana ingeendelea tungeaibika,” alisema Nchimbi.
Kwa upande wake bahati Lumato alisema kuwa msimu huu timu ya Yanga imewaumiza sana mashabiki wake kutoka ubingwa hadi nafasi ya pili. Hivyo ameushauri uongozi kuachana kabisa na kutegemea udhamini wa mtu mmoja bali iwe na mfumo wa kujiendesha kama kampuni.
“Mpira kwa sasa ni pesa na Yanga inatakiwa iwe na mfumo wa kuweza kujiendesha kiuchumi  kwa kuwa na wanahisa na iachane kabisa na uendeshaji wa kizamani kwani ndio jambo linalotukwamisha pale mdhamini anapopata misukosuko,” alisema Lumato.
Kwa upande wake, Lema Robison aliweka zaidi matumaini yake makubwa katika mkutano mkuu wa Yanga unaotarajiwa kufanyika Juni 10 mwaka huu. Alisema kama ukienda vizuri na watu wakatoa ya kwao ya moyoni na maamuzi mazuri kufanyika mwakani, watakomboa kombe la mapema.
“Yanga ndio bingwa wa Tanzania mara nyingi zaidi na kama akishindwa basi angalau nafasi ya pili lakini leo nafasi ya tatu ni aibu kwetu. Niwaombe wajumbe wanaokwenda kuhudhuria mkutano huo wawakilishe vyema na watoke na suluhu ya namna bora ya uendeshaji wa timu. Pia wachague watu sahihi wasiotetea matumbo yao kwa mgongo wa klabu,” alisema Lema.
     

No comments

Powered by Blogger.