Full-Width Version (true/false)


Mnyauko fusari kuhatarisha uchumi wa Mtwara
 
Moja ya zao la kimkakati katika sekta ya kilimo nchini ni korosho ambalo linaingizia pato kubwa serikali na wakulima, korosho imeendelea kuwa kitega uchumi kwa wananchi wa mikoa ya kusini hususani Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Zaidi ya 95% ya shughuli za maendeleo kwa wananchi wa kusini zinaendeshwa kwa kutegemea biashara ya korosho inayofanyika kwa mwaka mara moja, ambapo msimu wa
2017/2018 hadi kufikia mnada wa 10 Mkoa wa Mtwara ulikuwa umeongoza kwa kuuza zaidi ya tani 178,165.741 zenye thamani ya sh.701,674,466,366.00 kwa mujibu wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Bw. Jarufu.

“Mkoa wa Mtwara umeongoza kwa kuuza tani 178,165.741 zenye thamani ya sh. 701,674,466,366.00 ukifuatiwa na mkoa wa Lindi ambao umeuza tani 68,687.504 zenye thamani ya sh. 247,163,294,296.00. na Mkoa wa Ruvuma umeuza tani 19,545.613 zenye thamani ya sh. 76,173,400,063.00 na mkoa wa Pwani umeuza tani 19,429.347 zenye thamani ya sh. 57,189,224,856.00 na kufanya mapato yote kwa mwaka huu kufikia sh. trilioni 1.082 na minada bado inaendelea” alisema.


 
Pamoja na zao hilo ambalo limeonesha kuwa sehemu ya kuinua uchumi wa nchi hadi kuundiwa mpango wa miaka mitatu unaoratibiwa na Bodi ya korosho wa kupanda mikorosho 10,000,000 kila mwaka ili kuongeza uzalishaji kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa kilimo naliendele na sekretarieti za mikoa na Halmashauri za wilaya.

Mpango mkakati huo umekutana na changamoto kubwa sana kutokana na kugundulika kwa ugonjwa hatari sana unaoshambulia mashina, machipukizi na hata punje unaosababishwa na vimelea vya fusari.

Mnyauko fusari ni ugonjwa wa ukungu ambao unaenezwa na vimelea aina ya uyoga vinavyojulikana kama fusarium Oxysporum vinavyojificha katika udongo wa mikorosho iliyoathirika, ili kuepuka ugonjwa huo wakulima wanatakiwa kusafisha majembe yao baada ya kuyatumia pamoja na kutopanda miche kutoka katika mashamba mengine.


 
Uligundulika mwaka 2012 wilaya ya mkuranga na baadae kusambaa katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ambapo hadi hivi sasa imeua zaidi ya mikorosho elfu 40, kwa sasa ugonjwa huo hauna dawa na kinachofanyika ni kuendelea kutoa elimu kwa wakulima ili kuwasaidia kuzuia kusambaa kwake.
Mtaalamu wa kilimo akitoa maelezo juu ya Mnyauko Fusari.

Aidha taarifa ya kitaalamu kutoka kituo cha utafiti wa kilimo naliendele imeweza kuzitaja baadhi ya dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na majani katika baadhi ya matawi ya mkorosho kupoteza rangi yake ya kawaida ya kijani na kubadilika kuwa njano na baadaye kuwa kahawia.

“Machipukizi yaliyoshambuliwa na ugonjwa huu hunyauka, na majani hubadilika na kuwa na rangi ya kahawia, Matawi na mashina yakishambuliwa hunyauka na kufa, ukitaka kuthibitisha dalili za fusari kata shina utaona miviringo ya kahawia (Brown ring)” alieleza Dkt. Shomari.

Aliendelea kusisitiza kuwa mnyauko fusari unashamiri kwenye mashamba ambayo hayatunzwi vizuri, Viini vya ugonjwa huu vinauwezo mdogo wa kushambulia mkorosho wenye afya nzuri, ukiona shamba limeshambuliwa na uonjwa huu jua moja kwa moja kwamba shamba hilo halitunzwi vizuri kwa kufuata kanuni za kilimo bora.

Namna bora ya kuzuia mnyauko fusari ni kufanya palizi mara kwa mara, ukataji sahihi wa matawi, matumizi ya mbolea kwa kiwango kinachoshauriwa, kung’oa na kuchoma moto mikorosho iliyokufa, kupasha moto vifaa vinavyotumika kukatia mkorosho uliothibitika kuwa na mnyauko fusari.

Wananchi lazima watambue kuwa Korosho ni Miongoni mwa Mazao ambayo yamekuwa yakiinufaisha Jamii ya Wakulima na Kuliingizia taifa Mapato, ambapo Katika Mwaka fedha
2017/2018 Zaidi ya Shilingi Trilioni 1 Zilipatikana, kwahiyo wazingatie ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kuepuka kuingia katika umaskini.

Serikali imetoa tahadhari Juu ya kutokea kwa Ugonjwa wa MNYAUKO FUSARI Kwenye Zao la korosho na kutaja kuwa upo uwezekano wa kuathiri ustawi wa zao hilo la biashara ambalo linaonekana kufanya vizuri kwenye Soko la Dunia.

No comments

Powered by Blogger.