Full-Width Version (true/false)


MO Ibrahim ataka milioni 70 kubaki Simba

 

UONGOZI wa Simba unahitaji kumbakisha kiungo wa timu hiyo, Mohammed Ibrahim ‘Mo Ibra’, ambaye amehitaji shilingi milioni 70 ili aweze kuongeza mkataba mwingine ndani ya kikosi cha mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara. 

Mo Ibra msimu huu hakupata nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya kikosi cha Mfaransa Pierre Lechantre, kutokana na kudaiwa kuwa na nidhamu mbovu, lakini uongozi wa Simba umeziba masikio na kutenga dau la shilingi milioni 50 kumwongezea mkataba. Kiungo huyo amekuwa akitajwa kutakiwa na timu za Yanga na Singida United kwa ajili ya kupata huduma yake. 

Akizungumza na BINGWA jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa mchezaji huyo, Jamal Kisongo, alisema wiki mbili zilizopita alikutana na vigogo wawili wa Simba kwa ajili ya mazungumzo ya kujadili mkataba mwingine wa mteja wake. 

Alisema hakuna timu iliyokwenda kwao kwa ajili ya kuhitaji huduma ya mchezaji huyo zaidi ya Simba na kwamba, kama kuna timu inamhitaji na kuweka fungu kubwa la fedha zaidi ya Simba, atakuwa tayari kumruhusu. 

“Hadi sasa ni Simba tu ambao nimezungumza nao, wameweka mezani ofa ya shilingi milioni 50, lakini nilipokutana na Mo Ibra, alihitaji shilingi milioni 70, nasubiri arudi (kutoka Songea ambako Simba ilicheza na Majimaji jana) ili tuzungumze kama ataamua kubaki kwa ofa ya Simba, japo anatakiwa kubadilika na kuzaliwa upya,” alisema. 

“Kama Singida, Yanga na timu nyingine zitakuja na ofa kama ya Simba au pungufu ya hiyo, tutakaa na kuzungumza, lakini mwenye maamuzi ya mwisho ni mchezaji mwenyewe ambaye anaamua wapi aende,” alisema Kisongo.

No comments

Powered by Blogger.