Full-Width Version (true/false)


Mwanafunzi wa chuo kikuu (Duce) alalamika kuwekwa wodi ya vichaa wakati hana matatizo ya akili.

Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce), Emijidius Cornel ameulalamikia uongozi wa chuo hicho kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako alifikishiwa wodi ya wagonjwa wa akili wakati siyo mgonjwa wa akili.

Hata hivyo MNH kupitia kwa mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Aminiel Aligaesha alisema jana, “wataalamu wetu waliona huyo anafaa kulazwa wodi ya wagonjwa wa akili.”

Malalamiko ya Cornel
Cornel ambaye ni mratibu wa Umoja wa Wanafunzi wa Duce wanaotumia muda wao wa ziada kujitolea kufundisha katika shule za msingi na sekondari jijini Dar es Salaam, alisema jana kuwa ameshangazwa na tukio la kupigwa na askari wanaolinda chuo hicho lilivyobadilika na kuwa tatizo la maradhi ya akili. Akizungumzia namna sakata hilo lilivyoanza, alisema mwanafunzi mwenzake aliyejiunga katika umoja wao alitaka kujiondoa na alikuwa akidai michango yake.

“Wakati nafuatilia kumrudishia huku nikiendelea na masomo, alikwenda kushtaki kwa askari wanaolinda hapa chuoni ambao walinikamata na kunipiga.

“Waliponipiga nilikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Chang’ombe na niliporudi chuoni kwa ajili ya matibabu nikaanguka na wakanipeleka Hospitali ya Temeke kwa gari la wagonjwa,” alisema Cornel.

Alifafanua kuwa alipofikishwa katika hospitali hiyo alitibiwa na kurudi chuoni, lakini siku iliyofuata wauguzi wa zahanati ya chuo walimtaka kurudi naye Hospitali ya Temeke kuchukua nyaraka zake.

Alisema walikwenda naye na gari la wagonjwa na alipopata hizo nyaraka na kurudi chuoni hakuruhusiwa kushuka ndani ya gari.

“Nikafungwa pingu na kupelekwa Muhimbili kwenye wodi ya vichaa, na tulipofika wakasema hawawezi kunipokea na pingu kwa sababu mimi siyo mhalifu.

“Hivyo nipelekwe mahakamani itolewe hati ya mahakama ili nipokelewe, wakaenda mahakamani sifahamu mahakama gani wakaja na hati ya mahakama (court order) ndiyo nikafunguliwa pingu na kupokewa, ” alisema mwanafunzi huyo.

Alisema alikaa hospitalini hapo kwa muda wa siku 20 bila kuangaliwa na uongozi wa chuo wala askari waliompeleka, na familia yake ilipata taarifa kutoka kwa marafiki zake baada ya siku ya sita.

“Nilikaa na watu wenye matatizo ya akili nikilala nao, nikila nao kwa shida kwa siku 20 nikiwa mzima wa afya na bima yangu ikitumika kunihudumia ilhali siumwi. Madaktari walikuwa wakinipa dawa nikipata nafasi nazitupa au nazificha chini ya godoro, wakinibana sana ninazinywa na zilikuwa zinanichosha sana, ”alisema. Alisema baada ya kipindi chote hicho aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo na taarifa ya daktari ikaonyesha hakuwa na maradhi ya akili kama ilivyodaiwa.

Akizungumzia suala hilo, mjomba wa Cornel aitwaye John Kamugisha alisema hajawahi kuwa na historia ya matatizo ya akili.

Alisema alimtoa mkoani Kagera kwa dada yake kwa ajili ya kumsomesha jijini Dar es Salaam ambapo alisoma tangu darasa la kwanza hadi kidato cha sita katika shule za Mgulani, Kibasila na Benjamini Mkapa.“Huo ni mfano tu, kijana wangu amekuwa akijiongeza mwenyewe na kufaulu hadi kufikia hapo. Nasisitiza hakuwahi kuwa na tatizo la akili,” alisema Kamugisha.

“Iliniuma sana nilipompelekea chakula wakati anataka kuanza kula mmoja wa wagonjwa kwenye ile wodi akiwa amelowana haja ndogo na mikono michafu alikuja kujiunga kula na kijana wangu.

“Ninaomba haki itendeke, tujue lengo la wao kufanya hivyo lilikuwa nini, kwa sababu gani kijana wangu alikaa wodini siku 20 ndiyo anatolewa kwa maelezo kuwa haumwi kitu.”Majibu ya Muhimbili

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Hospitali ya Muhimbili, Aligaesha alisema hospitali hiyo inapokea wagonjwa mbalimbali ambao huhudumiwa kulingana na hali wanayokwenda nayo.

Alisema kwa kawaida madaktari huchukua vipimo, historia ya mgonjwa na kufanya tathmini kulingana na hali aliyofika nayo, kisha huamua wapi mgonjwa huyo alazwe.

“Sisi tutajua utalala wapi. Huwezi kutoka nyumbani unaumwa ukasema unataka kulala wodi ya wanawake, madaktari ndiyo tunaamua mgonjwa analala wodi gani,” alisema Aligaesha.

Hata hivyo alisema kama Cornel anaona hakuridhika na matibabu hayo na kule alikolazwa ana uhuru wa kukata rufaa kwa waziri wa Afya.

Duce waeleza hali ilivyo
Akizungumzia sakata hilo, mkuu wa Duce, Profesa Godliving Mtui alitaka kuandikiwa maandishi ili atoe ufafanuzi akidai kuwa tayari limefika mbali.

“Tuandikieni barua rasmi. Hili suala limefika mbali, hivyo hatutaki kulizungumzia kwa njia ya simu, bali kwa maandishi na kuwapa nakala Baraza la Habari ili mtu akitaka kutuhukumu, atuhukumu kwa barua hizo,” alisema

No comments

Powered by Blogger.