Full-Width Version (true/false)


Mwendokasi yawa mwiba, wananchi wadai daladalaWakazi wa Kimara jijini Dar es salaam, wamelalamikia usafiri wa mabasi ya mwendokasi kwa huduma hafifu wanazotoa, hususani nyakati za asubuhi na jioni, huku wakidai kwamba iwapo wameshindwa kuendesha mradi huo iwarudishie mabasi ya daladala.
Wakizungumza na www.eatv.tv, wakazi hao ambao walikuwa wamejazana kituo cha Kimara mwisho kusubiri usafiri wa mwendokasi, wamesema mabasi hayo yamekuwa machache na huku mengine yakionekana kuwa na mgomo baridi, na kusababisha watu kujaa kituoni.

Kwa upande mwengine wananchi hao wamemlalamikia supervisor wa mradi huo kituo cha Kimara kwa kitendo cha kutoa mabasi na kuruhusu kwenda kupakia watu wazima, na kuacha watu wa makundi maalum bila usafiri na kuwasababisha kukaa kituoni muda mrefu mpaka wengine kuanguka na kupoteza fahamu.

“Yaani hawa mwendokasi hawaeleweki, jana usiku tumekaa kituoni muda mrefu watu wamegoma kuja Kimara, akatokea dereva mmoja akatuonea huruma ndio akatoa basi, lakini walikuwa wamegoma, na hapa kama unavyoona huyu supervisor anaruhusu mabasi yote yakapaki kule mbele kwa watu wenye uwezo wa kugombania, sisi huku hatuna magari tumejazana kama unavyoona, yote yanapita yanaenda kule, sasa kama wameshindwa watuambie bora wangeturudishia daladala zetu”, amesema mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma Kindulanga.

Mwananchi mwengine aliendelea kuelezea aisema ….”Angalia wanafunzi wanavyopata shida mpaka wengine wanazimia hapa, magari hayaji, na yule baba magari yote anayaamrisha yaende kule mbele,yaani akikaa huyu tu hapa usafiri lazima uwe wa shida”, amesikika mkazi hyo wa Kimara.

Hii sio mara ya kwanza kwa wananchi kulalamikia usafiri huo wa mwendokasi, ambao mara nyingine umekuwa ukikumbwa na changamoto ya kuharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, na kusababisha mabasi kuwa machache na wananchi kukosa usafiri kwa muda mrefu.

Hata hivyo wwww.eatv.tv ilifanya jitihada za kuwatafuta watu wa UDART na kumpata Mkuu wa Idara mawasiliano UDART, ambaye alikiri kuwepo kwa changamoto ya uchache wa magari, na kusema kwamba tatizo hilo limetokana na magari mengi kuharibika kutokana na mvua zinazonyesha, lakini imeshaleta mabasi mapya ambayo yanasubiri kibali ili yaweze kuingia barabarani na kutoa huduma. 

"Tatizo la watu kujaa vituoni wakikosa usafiri kutokana na uchache wa mabasi sisi kama uongozi limetuumiza muda mrefu, na pia abiria wanapojaa kupita kiasi wanafanya mabasi yachoke haraka, tukafanya mpango wa kuleta mabasi mapya, tukaleta mabasi 70 hapa kibali kutoka kwa wakala wakishatupatia tu kibali tunaingiza magari barabarani”, amesema Bw. Deus  Bugaiwa.

No comments

Powered by Blogger.