Full-Width Version (true/false)


Ndani ya saa 24 waweza kukopeshwa Sh100 milion


Benki ya CRDB imetangaza punguzo la riba kwa mikopo ya wafanyakazi kutoka asilimia 22 hadi asilimia 16 ili kurahisisha upatikanaji na kufanikisha mipango waliyojiwekea.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Charles Kimei amesema benki imeamua kupunguza riba ili kutoa unafuu wa mikopo kwa wateja wake jambo litakalosaidia kuchochea kukua kwa kipato cha mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa zima kwa ujumla.

“Riba imekuwa kilio cha muda mrefu na kuchangia wengi kuogopa kukopa. Leo nina furaha kuwatangazia tumepata suluhisho,” amesema Dk Kimei.

Mbali na kupunguza riba, benki hiyo pia imeongeza kiwango cha kukopa kutoka Sh50 milioni hadi Sh100 milioni huku muda wa kurejesha nao ukiongezwa kutoka miaka nne mpaka saba.

Kwa wateja wanaodaiwa, iwe na benki hiyo au taasisi nyingine, amesema CRDB inao utaratibu wa kununua madeni hayo ili kuwapa wafanyakazi fursa ya kukopa zaidi.

Watumishi waliotimiza masharti, watapata mikopo yao ndani ya saa 24 tangu walipokamilisha utaratibu wa kuomba.

“Jukumu letu ni kuhakikisha mteja anapata huduma zinazokidhi mahitaji yake na zinazoendana na wakati,” ameongezea mkurugenzi huyo.

Punguzo hilo la riba ni kwa watumishi wa sekta zote mbili; za umma na binafsi.

Dk Kimei amebainisha zaidi kuwa kiwango cha chini cha mshahara kinachoruhusiwa kupata mkopo ni Sh200, 000 kwa mwezi.

CRDB ilianzishwa mwaka 1996 ikiwa na matawi 255 hivi sasa pamoja na mawakala 3,286.

Kadhalika CRDB ni miongoni mwa benki zilizotangaza kushusha gharama za marejesho ya mkopo kwa wateja wake hivi karibuni.

Taasisi nyingine zilizofanya hivyo ni Benki ya Afrika (BoA) inayotoza asilimia 11 kwa watumishi wa Serikali na mkopo kuanzia Sh1milioni mpaka Sh30 milioni na NMB inayotoza riba ya asilimia 17.
     

No comments

Powered by Blogger.