Full-Width Version (true/false)


Neymar na Gabriel Jesus wapewa majukumu haya timu ya Taifa

 KOCHA wa timu ya Taifa ya Brazil, Tite anaandaa moto mkali wa mastraika watatu, Neymar, Willian na Gabriel Jesus kwani ndio anaotaka waongoze mashambulizi ya timu hiyo wakati wa fainali za Kombe la Dunia.


Brazil na bingwa mtetezi, Ujerumani ndiyo zinapewa nafasi kubwa ya kuibuka kidedea kwenye fainali hizo zinazoanza kupigwa Juni 14, mwaka huu nchini Urusi.


Tite alianza kuwafanyisha mazoezi maalum nyota hao watatu juzi Alhamisi na kuashiria kuwa ndiyo safu anayotaka kuitumia wakati wa michuano hiyo.


Brazil imeanza mazoezi kwenye Uwanja wa Granja Comary uliopo nje kidogo ya Rio de Janeiro.


Pia Tite aliwatumia mabeki Marquinhos na Miranda kwenye kikosi chake ambacho kinaaminika ndiyo cha kwanza kwenye mazoezi hayo.


Willian anatazamiwa kuanza kwenye kikosi cha kwanza huku kiungo Renato Augusto akitakiwa kuanzia benchi.


Neymar naye anaendelea vizuri na mazoezi ambapo ameanza kuchezea tena mipira baada ya kuwa majeruhi tangu Februari, mwaka huu.


Brazil imepangwa Kundi E kwenye Kombe la Dunia ambapo itacheza mechi yake ya kwanza Juni 17 dhidi ya Uswisi.

No comments

Powered by Blogger.