Full-Width Version (true/false)


NINJE ATUPIWA LAWAMA BAADA YA KUMUWEKA BENCHI KABWILI
Kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, Ammy Ninje, ametupiwa lawama na baadhi ya mashabiki wa soka nchini kufuatia kikosi chake kufungwa mabao 2-1 na Mali.

Ngorongoro wamekubali kichapo hicho katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana ikiwa ni kuelekea kufuzu mashindano ya AFCON (U20).

Baadhi ya mashabiki wameeleza kuwa Ninje amekula jeuri yake kutokana na kutompanga Mlinda Mlango Ramadhani Kabwili na badala yake kumuweka langoni kipa kutoka JKU ya Zanzibar, Peter Mashauri.

Wapo wanoamini kupoteza kwa Ngorongoro jana ni kutokana na kiwango dhaifu cha Mashauri huku wakieleza Kabwili ana uzoefu.

Ninje alimuondoa Kabwili kwenye kikosi hicho siku za hivi karibuni akieleza alichelewa kufika kambini huku Yanga wakimsafirisha kuelekea Algeria kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger.

Licha ya kutemwa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Rais wake, Wallace Karia, ulimrejesha kikosi Kabwili lakini Ninje hakuweza kumpanga kwenye mechi ya jana.

Matokeo hayo yanailazimu Ngorongoro kushinda mabao 2-0 ili kusonga mbele katika mchezo wa marudiano utakaopigwa huko Bamako.

No comments

Powered by Blogger.