Full-Width Version (true/false)


PLUIJM AWAVUTA DANTE, KASEKE, TINOCO AZAM


 

WAKATI Azam ikitarajiwa kumpokea kocha wao mpya, Mholanzi Hans van der Pluijm, kumekuwa na utitiri wa wachezaji wanaotajwa kusajiliwa na timu hiyo ikiwa ni mapendekezo yake. 

Pluijm ambaye anainoa Singida United kwa sasa, anatarajiwa kuachana na timu hiyo mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara na mechi ya fainali ya Kombe la Azam Federation (AFSC), Juni 2, mwaka huu na tayari uongozi wa timu hiyo umeweka wazi juu ya kuondoka kwake. Hadi sasa Azam imeshaingia mkataba wa awali wa makubaliano na aliyekuwa straika wa Yanga, Donald Ngoma, kwa ajili ya msimu ujao, huku taarifa zikisema usajili wake ni kutokana na mapendekezo ya Pluijm. 

Mbali na mchezaji huyo, lakini pia taarifa zilizopo ni kwamba, uongozi wa Azam upo katika mazungumzo na beki wa kati wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’, ikiwa ni kuboresha kikosi chao lakini pia ni moja ya mapendekezo ya Pluijm. 

Taarifa kutoka ndani ya Azam zinasema, kocha huyo amependekeza wachezaji kadhaa ambao anawahitaji katika kikosi chake, akiwemo pia Deus Kaseke na Tafadzwa Kutinyu ambaye tayari ameshamalizana na Wanalambalamba hao, lakini pia ameelekeza jicho lake kwa Benedict Tinoco. 

“Tangu akiwa anainoa Yanga, ni wazi kuwa Pluijm ni kocha anayemkubali sana Ngoma, ndiyo sababu amefanikisha usajili wake, lakini pia yupo Dante, Kaseke na Kutinyu ambaye tayari ameshasaini mkataba wa mwaka mmoja ndani ya Azam“Lakini pia Azam wameamua kumpandisha basi kipa namba moja wa Mtibwa Sugar, Tinoco, kuja Dar es Salaam kumalizana naye,” alisema mtoa habari huyo. 

BINGWA lilizungumza na Tinoco ambaye alithibitisha kuwa tayari wameshafanya mazungumzo na Azam FC na kukubaliana asaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo msimu ujao. 

“Mazungumzo ya mkataba yameshamalizika na kesho au keshokutwa (leo au kesho), nitakuja Dar es Salaam kusaini tu kisha kurejea Mtibwa kumalizia majukumu yangu katika fainali Kombe la Azam Federation tutakapocheza na Singida United. 

“Najua Azam nitakutana na ushindani kwani hadi sasa kuna makipa watatu tayari, lakini hilo halinipi hofu ninahitaji changamoto mpya katika sehemu ambayo kutakuwa na ushindani,” alisema. 

Azam imeamua kujiimarisha kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara wakianzia maboresho hayo katika benchi la ufundi, kwa kumleta kocha huyo mwenye uzoefu na michuano hiyo nchini lakini pia kuongeza nguvu katika kikosi chao.

No comments

Powered by Blogger.