Full-Width Version (true/false)


“Polepole atanifundisha siasa”-BashiruKatibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ali amesema itachukua muda kujifunza masuala mengi ya siasa za chama hicho na jinsi ya kuongea na vyombo vya habari kutoka kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole. 

Dkt. Bashiru amesema hayo leo Mei 31, Ofisi ndogo za CCM Lumumba, Jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa Ofisi na vitendea kazi na mtangulizi wake Abdulrahman Kinana na kuongeza kuwa yeye ni mchambuzi wa siasa lakini sio mzungumzaji sana kama viongozi wengine.

“Humphrey (Polepole) ni mwenyeji kidogo anifundishe namna ya kuzungumza na vyombo vya habari masuala ya siasa ya chama tawala, mimi nilikuwa ni mchambuzi, napiga nondo za sayansi ya siasa, sasa lazima niingie msituni kujifunza namna gani naweza kuzungumza kama mzungumzaji wa chombo cha utendaji cha chama” amesema Dkt. Bashiru

Dkt. Bashiru ameongeza kuwa kama chama tawala kinawajibu wa kutoa ufafanuzi kwa wananchi kuhusiana na mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya chama hicho na kuwataka watendaji wengine wa CCM kujenga ukaribu na vyombo vya habari.

Mapema leo Mei 31, 2018 Dkt Bashiru alikabidhiwa Ofisi rasmi katika nafasi ya ukatibu mkuu wa CCM baada ya kuchaguliwa katika kikao cha Halmashauri kuu taifa (NEC) Jumanne Mei 29, 2018.

No comments

Powered by Blogger.