Full-Width Version (true/false)


Rais Magufuli amefanya mabadiliko ya kiutendaji katika Wizara tatu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo May 10, 2018 amemuapisha Alphayo Japani Kidata kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada na  Msalika Robert Makungu kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora.

Balozi Kidata ambaye pia ataiwakilisha Tanzania nchini Cuba anachukua nafasi iliyoachwa na  Balozi Jack Mugendi Zoka ambaye amemaliza muda wake, wakati Makungu anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Thea Ntara ambaye amestaafu.

Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amewapongeza kwa uteuzi huo na kuwataka kwenda kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kwa manufaa ya Taifa.

Rais ameelezea kusikitishwa kwake na kutotekelezwa kwa maagizo aliyoyatoa kwa Mabalozi wote kumpa taarifa juu ya utendaji wao wa kazi na manufaa ambayo Tanzania imeyapata kwa uwepo wa kila Balozi katika nchi aliyopangiwa kila robo mwaka.

“Nataka nijue katika kipindi ambacho Balozi ameteuliwa kuiwakilishi Tanzania katika nchi fulani, nchi imenufaikaje na uwepo wake kwenye nchi ile? Kuteuliwa sawa lakini sio lazima ukae katika ubalozi huo kwa kipindi chote ulichopangiwa, ukishindwa kuleta manufaa unarudishwa na huko anapangiwa mtu mwingine atayeleta manufaa kwa nchi” amesema Rais Magufulli.

Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kufanya kazi nzuri katika sekta ya elimu na afya lakini ameelezea kutoridhishwa na utendaji katika sekta maji na ardhi kutokana na usimamizi mbaya wa miradi mingi ya maji na usimamizi mbaya wa masuala ya ardhi na mipango miji.

Rais Magufuli amesema tangu mwaka 2010 Serikali imetoa Shilingi Bilioni 109 kwa ajili ya miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini, lakini uchunguzi umeonesha miradi iliyotekelezwa ipasavyo na kuonesha thamani halisi ya fedha zilizotumika, ni ya Shilingi Bilioni 17 tu.

Kufuatia hali hiyo Rais Magufuli ameagiza wataalamu wote wa idara za maji katika halmashauri zote nchini wasimamiwe moja kwa moja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji na wataalamu wa ardhi na mipango miji katika halmashauri zote nchini wasimamiwe na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kuimarisha usimamizi wa shughuli zinazofanywa na idara hizo na kuwawajibisha wahusika pale mradi unapotekelezwa visivyo.

“Sasa hivi kila mahali watu wanalalamikia maji, wabunge wanalalamika, wananchi wanalalamika, Serikali imetoa fedha lakini miradi haitoi maji, ukichunguza miradi hii inasimamiwa na wahandisi wa maji wa halmashauri ambao Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ambaye ana wataalamu wa maji hana uwezo wa kuwawajibisha, wahandisi wanawajibika kwa madiwani, sasa hatuwezi kwenda kwa mtindo huo.

“Vivyo hivyo kwenye ardhi kuna matatizo mengi ya ardhi na mipango miji, watu wanadhulumiwa ardhi, ugawaji wa viwanja ni matatizo, maafisa ardhi  na mipango miji wanachelewesha vibali vya ujenzi, huku nako Katibu Mkuu wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi hana mamlaka ya kuwachukulia hatua, hili nalo tatizo” amesisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amemtaka Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo kukutana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Isack Kamwele na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi kutengeneza muundo utakaozingatia maelekezo hayo.

No comments

Powered by Blogger.