Full-Width Version (true/false)


Rais Magufuli apongezwa kwa mipango ya serikali


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amepongezwa kwa mipango ya serikali yake katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo suala la kusikiliza kero yeye mwenyewe anapokuwa kwenye ziara zake.

Akizungumza kwenye kipindi cha  East Africa BreakFast kinachorushwa na East Africa Radio, mchambuzi wa siasa za kikanda Amini Mgeni, amesema Rais Magufuli ameweza kujitofautisha na viongozi wengine kwa kuwapa fursa wananchi na wabunge wakiwemo wa upinzani kuelezea matatizo yao.

“Tumeshuhudia mara kadhaa Rais akiwa kwenye ziara yake, anawapa nafasi wananchi waeleze shida zao, nakisha yeye mwenyewe anatoa maelekezo ya nini kifanyike, hii ni mbinu ya kiuongozi ambayo inamfanya ajenge imani kubwa kwa wananchi na viongozi wao” ameeleza Amini.

Hivi karibuni Rais Magufuli akiwa kwenye ziara yake mkoani Morogoro alishuhudiwa akimpa nafasi Mbunge wa Mikumi Joseph Haule (CHADEMA), pamoja na Mbunge wa Kilombero Peter Lijuakali (CHADEMA) ili waeleze changamoto zao, suala ambalo Amini analitaja kuwa ni njia nzuri ya kuleta mshikamano na kurahisisha utatuzi wa kero za wananchi.

“Ni mnyororo wa kiuongozi ambao unaleta tija katika kutatua changamoto kwenye jamii badala ya wananchi kubaki na matatizo yao, wakikosa pakueleza, watakuwa wakifikisha kwa viongozi wao wakiamini kuwa zitafika kwa mkuu wa nchi nakutatuliwa haraka” amefafanua Amini.

No comments

Powered by Blogger.