Full-Width Version (true/false)


REKODI HIZI HAZIWEZI KUVUNJWA KOMBE LA DUNIA…


 
SIKU 16 zimesalia kabla ya fainali za Kombe la Dunia kuanza kutimua vumbi nchini Urusi, katika kipindi hiki ambacho ligi mbalimbali zimemalizika barani Ulaya, kila shabiki wa soka anasubiri michuano hiyo kwa hamu kubwa.
 
Tangu kuanza kwa fainali hizo mwaka 1930, kumekuwa na mabadiliko mengi katika mpira ikiwamo baadhi ya sheria na kanuni, lakini kivutio zaidi mwaka huu ni teknolojia ya video inayomsaidia refa katika maamuzi.

Timu 32 zinazotarajiwa kutoana jasho zimejipanga kikamilifu kuhakikisha wanafanya vizuri na hatimaye kushinda kombe hilo.

Tangu mwaka 1930, rekodi nyingi zimewekwa katika fainali hizo lakini zipo zilizovunjwa na nyingine kukaribia kuvunjwa, ila hizi ambazo tunakuletea leo haziwezi kuvunjwa kwa urahisi.

KADI TATU ZA NJANO
Inaonekana umeshangaa sana baada ya kuona hizo kadi tatu za njano. Beki wa Croatia, Josip Simunic, anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyeonyeshwa kadi tatu za njano kabla ya kutolewa kwa nyekundu na refa Ghaham Poll katika mchezo dhidi ya Australia.

Simunic alipewa kadi dakika ya 61, 90 na 93. Refa wa mchezo huo alisahau kuandika kadi ya kwanza kwenye kumbukumbu zake.

KOCHA MDOGO ZAIDI
Miaka ya karibuni makocha vijana wamekuwa wakiibuka kila siku, lakini katika fainali za Kombe la Dunia, kocha wa Argentina, Juan Jose Tramutola, anashikilia rekodi ya kuwa kocha mdogo zaidi kuongoza timu, alikuwa na miaka 27 na siku 267.

Ilikuwa katika fainali za mwaka 1930 zilizofanyika nchini Uruguay. Miaka ya sasa ni ngumu kwa mashirikisho ya mpira kutoa kazi kwa kocha asiyekuwa na uzoefu.

MASHABIKI WENGI ZAIDI
Rekodi pekee ya kuingiza mashabiki wengi uwanjani katika fainali za Kombe la Dunia ilikuwa mwaka 1950, ndani ya Uwanja wa Maracana, nchini Brazil.

Uwanja huo uliingiza watu zaidi ya 170,000, katika mchezo wa fainali kati ya Brazil na Uruguay, ambapo Uruguay walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wao waliopewa nafasi ya kutwaa taji hilo.

ADHABU KUBWA ZAIDI
Nahodha wa Peru, Paolo Guerrero, hivi karibuni alikumbana na adhabu ya kufungiwa baada ya kuthibitika kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni kwa muda wa miezi 14.

Manahodha wa timu mbalimbali hivi karibuni waliungana kumuombea msamaha FIFA itengue adhabu yake ili aweze kukiongoza kikosi cha Peru katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, nchini Urusi.

Kipa Chile, Roberto Rojas’ alifungiwa maisha na Shirikisho la Soka Ulimwenguni, FIFA kujihusisha na mchezo huo kutokana na udanganyifu alioufanya katika fainali zilizofanyika mwaka 1990.

Rojas alidanganya amepigwa na muale wa baruti uliorushwa uwanjani, lakini pia alijichana kwa kiwembe katika mikono yake kuashiria aliumizwa na muale huo.

Mwaka 2000 alikiri kudanganya na alipewa adhabu ya kufungiwa maisha kujihusisha na soka.

Tangu adhabu hiyo itoke kwa mchezaji, FIFA haijawahi kutoa adhabu nyingine inayofanana na hiyo kwa wachezaji wakiogopa kuharibu maisha ya wachezaji.

No comments

Powered by Blogger.