Full-Width Version (true/false)


Ripoti ya Ukaguzi wa mali za CCM Yamuibua Makamba Afunguka Haya

Wakati joto la matokeo ya ripoti ya ukaguzi wa mali za CCM likianza kupanda, katibu mkuu wa zamani wa chama hicho, Yusuf Makamba amezungumzia mchakato wa uchunguzi, akibainisha kuwa alishiriki kutoa maoni wakati kamati hiyo ikifanya kazi hiyo.

Rais John Magufuli, ambaye aliunda kamati ya kufanya ukaguzi wa mali za chama hicho kikongwe nchini, alikabidhiwa ripoti hiyo juzi.

Baada ya kuipokea, Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM aliwaagiza wajumbe wa sekretarieti waliohudhuria hafla ya uwasilishaji wa ripoti hiyo kuanza kufanyia kazi mambo yaliyo ndani ya uwezo wao na kwamba masuala mengine yataamuliwa na vikao vya juu vya chama.

CCM inamiliki mali za aina tofauti kama viwanja vya michezo, majengo ya vitega uchumi, vituo vya mafuta, kumbi za mikutano, vyombo vya habari, maegesho ya magari yaliyoenea karibu nchi nzima, kumbi za starehe, mashamba na viwanja.

Habari zinasema kamati hiyo imebaini upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa na mikataba mibaya, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama.

Baadhi ya viongozi wa kitaifa wa CCM, mikoa na wilaya wanatajwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa huenda wakachukuliwa hatua kutokana na kuhusika katika vitendo hivyo.

Jana, Mwananchi liliongea na Makamba ambaye alikuwa katibu mkuu wa CCM kati ya mwaka 2007 hadi 2011, na ambaye inadaiwa kuwa alihojiwa na kamati hiyo kutokana na wadhifa wake kama mtendaji mkuu wa chama hicho.

“Walikuja kuchukua maoni kwangu,” alisema Makamba baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu utendaji wa kamati hiyo. “Walitaka kujua tulikuwa tunaendeshaje chama, fedha tulikuwa tunapata wapi, changamoto ni zipi na nini maoni yetu kuhusu chama kiendeshwaje.”

Makamba, ambaye amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema kamati haikumfuata ili kumhoji kama habari zilizoenea mitandaoni, bali kamati ilitaka maoni yake.

Lakini hakutaka kuzungumzia matokeo ya ripoti hiyo, zaidi ya kusema vikao vya juu ndivyo vitakavyojadili na kutoa uamuzi.

“Bado mapema mno,” alisema Makamba, ambaye pia aliwahi kushika nafasi mbalimbali katika chama na Serikali.

“Ripoti yenyewe imekabidhiwa tu, wala haikusomwa. Pili itakwenda kujadiliwa kwenye Kamati Kuu na baadaye kwenye (mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa) NEC na wahusika watajadiliwa.

“Wakibainika kuhusika, wataadhibiwa. Na mimi kama nimo nitaadhibiwa. Kwa hiyo huko ndiko sehemu sahihi. “Wasambaa wana msemo kuwa, ukiwa njiani unatembea ukaona majani yanacheza, usije ukaanza ah! ah! (sauti ya hofu) ukidhani ni mnyama simba, kumbe ni panya. Hivyo ngoja tuone kwanza kitakachotokea kwenye majani usianze ah! ah! wakati ni mbuzi.”

Kuhusu kamati hiyo kumfuata, Makamba alithibitisha kufuatwa na kwamba si yeye pekee, bali viongozi wengine waliowahi kushika nafasi kama yake na za kusimamia fedha.

Lakini akizungumza na Mwananchi baadaye jana mchana, Makamba alisema kwa nafasi yake kama katibu mkuu alikuwa hashiki fedha.

“Katibu mkuu hashiki fedha, ana wasaidizi wake ambao kama anasafiri huchukua fedha na anaporudi hu-retire (huwasilisha stakabadhi za matumizi),” alisema.

Makamba alisema kila mwezi chama hicho hufanya mikutano na kuna vikao vya kuandaa bajeti kwa ajili ya vikao. Pia alisema ndani ya chama kuna muundo mzuri wa uongozi, mhasibu mkuu na kuna mweka hazina ambao ndio wanashika fedha. Fedha inatoka kwa mweka hazina inakwenda kwa mhasibu mkuu.

“Kama wataniwajibisha, labda ni kwa sababu sikumchukulia hatua kiongozi wa mkoa ambaye aliletwa kwangu kwa kufanya kosa.”

Kuhusu tuhuma za uuzwaji kiholela wa mali za chama, Makamba alisema suala hilo linasimamiwa na Baraza la Wadhamini ambalo alisema huidhinisha uuzwaji au kukataa. Miongoni mwa tuhuma zinazotajwa juu ya mali za CCM ni uuzwaji kiholela wa mitambo ya uchapishaji magazeti ya Uhuru Publications Limited.

“Wanaotoa idhini ni Baraza la Wadhamini na wakati wangu mwenyekiti wa baraza alikuwa ni (anamtaja jina) na baadaye akawa (anamtaja jina),” alisema.

Kamati hiyo iliyofanya kazi kwa miezi mitano ilitembelea mikoa yote kukagua mali hizo ikiwamo kuwahoji wahusika wakiwamo vigogo na makada wa chama hicho.

Maeneo ambayo yameonekana kuzungumzwa zaidi na baadhi ya makada wa chama hicho ni jumuiya za chama hicho ambazo ni Wazazi, Wanawake (UWT) na Vijana (UVCCM).

No comments

Powered by Blogger.