Full-Width Version (true/false)


Rufaa ya Yanga kwa Mbeya City yagonga mwamba,"Hakuna namna yoyote ile mchezaji anayezidi kubadili matokeo"


Baada ya kutokea hali ya taharuki na malalamiko kwenye mchezo uliyochezwa mwishoni mwa mwezi Aprili kati ya Mbeya City na Yanga, leo hii Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Kamati ya saa ya Ligi imetupilia mbali shauri la Yanga la kutaka kupatiwa ushindi wa alama 3 na mabao 3.

Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam hii leo Mei 03, 2018 na kusema hakuna Kanuni yoyote ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayoweza kubadili matokeo ya uwanjani kwa mazingira ambayo Yanga imeyalalamikia ya kuwepo kwa mchezaji zaidi katika timu ya Mbeya City pindi walipokuwa wanacheza.

"Hakuna namna yoyote ile mchezaji anayezidi (extra player) kubadili matokeo ya mchezo. Katika mazingira ya 'extra player' likifungwa bao, mwamuzi atalikataa bao hilo. Kutokana na kanuni za Ligi kutojitosheleza katika suala hilo la 'extra player', Kamati iliangalia Kanuni za FIFA na kufikia uamuzi huo", amesema Wambura.

Aidha, Wambura amesema mchezaji Ramadhan Malima wa Mbeya City ambaye alitolewa nje kwa kadi nyekundu, lakini akatoka kwenye chumba cha kuvalia (dressing room) na kwenda kushangilia bao la kusawazisha la timu yake amesimamishwa hadi suala lake litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.

Kwa upande mwingine, Wambura amesema wameiandikia barua Kamati ya Waamuzi ya TFF kutoka na mapungufu yaliyojitokeza katika suala la kusimamia ubadilishaji wa wachezaji.

No comments

Powered by Blogger.