Full-Width Version (true/false)


Serikali kuchukua hatua hii kwa Wanafunzi
Serikali imeahidi kufuta matokeo ya wanafunzi pamoja na usajili wa vituo vyote vya mitihani nchini ambavyo itathibitika kuhatarisha usalama wa mitihani na kufanya udanganyifu kipindi cha kufanyika  mtihani wa taifa kidato cha sita utakaoanza kesho.

Akiongea na vyombo vya habari leo Mei 06, 2018 wakati wa kutangaza kuanza kwa mtihani wa taifa kidato cha sita, katibu mtendaji wa  wa baraza la mitihani nchini (NECTA) Dkt. Charles Msonde  amesema ikithibitika udangavyifu wa aina yoyote baraza litachukua hatua stahiki na kutoa wito kwa wamiliki na wakuu wa shule pamoja na walimu kutoingilia majukumu ya usimamizi wa mitihani hiyo.

“Wamiliki hawatakiwi kwa namna yoyote ile kuingilia majukumu ya usimamzi wa mitihani ya taifa, baraza halitasita kuchukua hatua thabiti ikiwemo kuvifuta vituo vyote vya mitihani hiyo endapo itabaini kwamba uwepo wake unahatarisha usalama wa mitihani” alisema Msonde

Sambamba na hilo Dkt.Msonde aliwataka wananchi  kuheshimu mipaka ya  vituo vya mitihani pamoja na kushirikiana na baraza hilo kwa kutoa taarifa endapo wataona dalili za watu ambao wanahatarisha usalama wa mitihani.

Kuanzia kesho Jumatatu, Mei 07 2018 ,  wanafunzi  wa kidato cha sita nchini wataanza mtihani wa taifa na kumalizika Mei 25,  ambapo jumla wanafunzi wa shule waliosajiliwa ni 77222 na watahiniwa wa kujitegemea ni 10421.

Pia kesho kutafanyika  mtihani wa taifa  kwa wanafunzi wa kozi ya ualimu ngazi ya cheti na stashada katika vyuo vya ualimu 125 Tanzania bara na Zanzibar. Jumla ya watahiniwa katika ngazi ya cheti ni 5234 na stashahada ni 2188.

No comments

Powered by Blogger.