Full-Width Version (true/false)


Serikali yaahirisha majibu kuhusu mafuta ya kula Hadi Kesho Jioni

Licha ya Spika wa Bunge Job Ndugai kuitaka Serikali leo jioni Mei 8, 2018 kutoa majibu kuhusu hali ya upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, imesema itatoa maelezo hayo kesho jioni.

Kufuatia hali hiyo Ndugai amesema, “Kesho saa 11 jioni Serikali ikiwa haitakuwa na majibu katika hili nitalifunga kiaina na kuwaacha wananchi.”

Ndugai ametoa kauli hiyo leo jioni baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama kusimama na kutoa kauli ya Serikali kuhusu suala hilo, akiomba jambo hilo kujibiwa kesho.

“Hivi sasa ni saa 12 jioni na kikao cha kupokea matokeo ya uchunguzi wa kisayansi kutoka taasisi husika kinaendelea na kinaongozwa na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa),” amesema.

“Baada ya kikao hicho kukamilika, ninaomba Bunge lako liridhie taarifa ya Serikali itolewe kesho jioni ili iwe taarifa kamilifu ya kutoa mwelekeo ya kutatua tatizo hilo.”

Asubuhi Ndugai alitaka majibu kuhusu madai ya kuadimika kwa mafuta yatolewe leo jioni baada ya majibu ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhusu suala hilo kutoridhisha.

Tishio la kuadimika kwa mafuta ya kula linatokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzizuia meli mbili zenye tani 62,000 za mafuta ya kula katika Bandari ya Dar es Salaam tangu mwezi uliopita kushusha mzigo mpaka wamiliki wake watakapolipa kodi husika.

Utata wa kulipa kodi inayodaiwa na TRA, unatokana na madai ya mamlaka hiyo inayosema mafuta yaliyoingizwa ni safi ilhali wamiliki wakieleza ni ghafi.

No comments

Powered by Blogger.