Sethi avuliwa ukurugenzi wa IPTL akiwa mahabusu
Huku
akikabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, Harbinder Sing Sethi
ameondolewa katika orodha ya wakurugenzi wa kampuni ya kufua umeme ya
Independent Power Tanzania (IPTL).
Uamuzi
wa kumuondoa Seth katika ukurugenzi umefikiwa na bodi ya wakurugenzi
ambayo pia imemvua madaraka ya kuwa mwenyekiti mtendaji wa IPTL, baada
ya kushindwa kushiriki na kuhudhuria mikutano ya bodi.
Seth
anadaiwa kushindwa kuhudhuria vikao vya bodi bila kuruhusiwa na
wakurugenzi wenzake kwa miezi sita mfululizo tangu Juni 19, 2017
alipokamatwa na kushitakiwa.
Hayo
yamo kwenye taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa
IPTL, Ambroce Lugenge wakati akitoa muhtasari wa maazimio yao wakati wa
mkutano mkuu wa tatu uliofanyika Aprili 10.
Mkutano
huo ulikuwa na ajenda kuu ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto
zinazoikabili kampuni hiyo na uendeshaji wa mambo yanayohusu IPTL.
Sethi
anakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na
kuisababisha Serikali hasara ya Dola22.198 milioni za Marekani na
Sh309.5 bilioni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kusutu.
“Bodi
ilijadili kuhusu kesi namba 27 ya 2017 ya uhujumu uchumi inayomkabili
ndugu Harbinder Sing Sethi na athari yake kwa kampuni, muundo wa
kiutendaji wa kampuni ikiwemo na uongozi, udhibiti na ushushaji wa
gharama pamoja na uwepo wa kesi mbalimbali mahakamani dhidi ya kampuni
au ya kufunguliwa na kampuni,” alisema Lugenge.
Taarifa
hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ilisema bodi ilimtunuku
Sethi ukurugenzi wa heshima kwa msingi kuwa “aliongoza” kampuni hiyo
kutoka katika hatari ya kufilisiwa kutokana na kesi iliyokuwa
imefunguliwa na kampuni ya VIP Engineering and Marketing kati ya mwaka
2002 hadi 2013.
Kutokana
na uamuzi huo, Sethi hataruhusiwa kwa namna yoyote ile kushughulikia
masuala yanayohusu kampuni hiyo au kuingia makubaliano yoyote kwa niaba
ya kampuni.
“Bodi
imeelekeza uongozi mpya, hasa menejimenti kuwafikia wadau ikiwa ni
pamoja na Serikali ili kuangalia namna bora ya kutatua madai yote dhidi
ya kampuni, ikiwemo hasara inayodaiwa kusababishwa na ndugu Sethi kwa
mamlaka husika, iliyopelekea kukamatwa na kushtakiwa kwake ibebwe na
kampuni na kuyatafutia ufumbuzi kwa masilahi ya umma,” alisema Lugenge
katika taarifa hiyo.
Pia,
alisema bodi imeagiza menejimenti mpya kukaa na Mamlaka ya Mapato ya
Tanzania (TRA) ili kubaini kodi stahiki na kuweka mazingira bora ya
kuzilipa haraka iwezekanavyo baada ya kubaini kiasi kisicho na
pingamizi.
Lugenge
katika taarifa hiyo alisema bodi hiyo imemteua Joseph Makandege kuwa
mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo ili kuongoza uboreshaji kiutendaji,
uteuzi ulioanzia Aprili 10.
Alisema
katika mkutano, bodi ilijadili na kufikia maazimio katika vipengele
vingine 10 vya ajenda, ambavyo vilikuwa vinachangia kwa kiasi kikubwa
kuamua mwelekeo na hatima ya kampuni hiyo.
No comments