Full-Width Version (true/false)


Sheik Mbonde: Nitatumia Mamilioni Kuhakikisha Babu Tale Anakaa Jela


Baada ya mkurugenzi wa kampuni ya Tiptop Connection Limited, Hamis Shaaban Taletale maarufu kwa jina la Babu Tale, kukaa mahabusu katika kituo cha Polisi akisubiri amri ya kupelekwa kifungoni, mdai katika kesi hiyo amesema atatumia mamilioni kuhakikisha anakaa jela.

Hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Augustine Shangwa Februari 18, 2016, iliamuru Babu Tale na ndugu yake Idd Taletale kumlipa fidia ya Sh250 milioni, Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde kwa makosa ya kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa yake.

Hati ya kuwakamata Babu Tale na ndugu yake ilitolewa Aprili 4, mwaka huu kutokana na maombi ya Sheikh Mbonde kupitia wakili wake, Mwesigwa Muhingo.

Sheikh Mbonde aliwasilisha maombi hayo baada ya Babu Tale na nduguye kushindwa kutekeleza hukumu hiyo, yaani kumlipa kiasi hicho walichoamriwa na Mahakama wala kubainisha mali za kampuni yao, au zao binafsi, ili zipigwe mnada kulipia fidia hiyo.

Baada ya Sheikh Mbonde kuwasilisha maombi ya kuwafunga jela Babu Tale na nduguye, mahakama ilimwelekeza kuwalipia wafungwa hao watarajiwa fedha za chakula na matumizi mengine kuziwasilisha gerezani.

Kwa mujibu wa Mahakama, gharama za kuwahudumia wafungwa hao wakiwa gerezani ni kama ifuatavyo:

Vifaa ambavyo ni taulo ya kuogea Sh12,000; godoro Sh40,000; mto wa kulalia Sh10,000; chandarua Sh13,000; mashuka manne Sh48,000; kandambili (malapa) Sh3,000; mswaki na dawa ya meno Sh2,000 ambazo jumla ni Sh128,000 kwa mtu mmoja na kwa watu wote wawili ni Sh256,000.

Chakula, kifungua kinywa Sh7,000; chakula cha mchana Sh8,000; maji lita tatu 3,000, jumla Sh18,000 kwa mtu mmoja kwa siku na kwa wote wawili ni Sh36,000. Wote kwa mwezi ni Sh1,080,000.

Pia, kuna fedha za tahadhari kiasi cha Sh800,000 kwa kila mfungwa na kwa wote wawili jumla ni Sh1,600,000.

Sheikh Mbonde alisema kuwa tayari ameshawalipia wafungwa hao fedha za chakula za mwezi mmoja kiasi cha Sh1,080,000 na kusema ataendelea kuwalipia kiasi kama hicho kila mwezi.

Alisema fedha za matumizi mengine kama yalivyoainishwa na mahakama, ziko tayari na kwamba hizo ataziwasilisha kwa uongozi wa gereza baada ya wafungwa hao kufikishwa huko.

No comments

Powered by Blogger.