Full-Width Version (true/false)


SIRI YA NGOMA KUTUA AZAM FC YAFICHUKA

 

BAADA ya straika wa zamani wa Yanga, Donald Ngoma kusaini Azam FC, siri imefichuka kwanini Mzimbabwe huyo akaamua kufanya kitendo hicho, wakati inajulikana ni majeruhi wa muda mrefu.

Uongozi wa Wanalambalamba hao umethibitisha kuingia makubaliano na Ngoma kwa ajili ya kumtumia msimu ujao wa 2018/19 na taarifa zaidi zinadai kuwa, muda wowote wanatarajia kumpeleka mchezaji huyo Afrika Kusini, kwa matibabu zaidi.

Mchezaji huyo amekabidhiwa jezi namba 11 kama ile aliyokuwa akiitumia Yanga, na kinachosubiriwa kwa sasa ni msimu ujao ambao Wanalambalamba hao wanajipanga kuhakikisha wanawapoka Simba ubingwa.

Taarifa zaidi zinadai kuwa, Azam FC walikuwa wameshafanya mazungumzo na Ngoma mwanzoni mwa msimu huu, ndiyo maana hata alipotajiwa na Yanga suala la kuvunja naye mkataba haraka sana alikubali.

Taarifa hizo zinadai kuwa, Ngoma hakuwa mgonjwa kiasi cha kumsababishia kukosa kuichezea Yanga michezo mingi msimu huu, lakini alifanya hivyo ili kurahisisha safari yake ya kutua Azam FC.

“Alijua kwamba bado anao mkataba na Yanga, hivyo angecheza isingekuwa rahisi kuuvunja, ndiyo maana akatumia ujanja huo wa kujifanya hajapona.

“Ili ujue kwamba ni mchezo uliochezwa, iweje Azam wakubali kumchukua mtu ambaye ni majeruhi wa muda mrefu? Kwa akili ya kawaida hilo haliwezekani, lakini kwa sababu ilishapangwa imetimia, ndiyo maana hata alipotakiwa kuvunja mkataba na Yanga alichangamkia dili hilo,” kilisema chanzo muhimu cha DIMBA.

Taarifa nyingine zinadai kuwa, Azam walishaambiwa na kocha Hans van der Pluijm, ambaye muda wowote naye atajiunga na kikosi hicho kuhakikisha wanamsajili Ngoma, ambaye ni kipenzi cha Mholanzi huyo tangu akiwa anaifundisha Yanga.

Tayari Singida United imeshatangaza kuachana na kocha huyo na kinachosubiriwa ni kuiongoza kwenye mchezo wa fainali wa michuano ya Azam, maarufu kama FA, dhidi ya Mtibwa Sugar, mchezo utakaochezwa mapema mwezi ujao, Uwanja wa Sheikh Amri Abedi, jijini Arusha.

No comments

Powered by Blogger.