Full-Width Version (true/false)


Uongozi UDSM wasitisha mchakato wa uchaguzi Daruso 
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umesitisha kwa muda mchakato wa uchaguzi wa uongozi wa wanafunzi (Daruso).

Akizungumza na MCL Digital leo Mei 31, 2018 Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Cuthbert Kimambo amesema kusitishwa kwa mchakato huo kumetokana na kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wagombea wa uchaguzi huo.

Amesema Mei 24, 2018 walipokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi wawili waliokuwa wanagombea nafasi ya urais.

Amefafanua kuwa katika malalamiko hayo wamesema kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.

“Malalamiko hayo yalipokelewa na baada ya kuyashughulikia kwa kina uongozi wa chuo umeelekeza wahusika kufuata taratibu zilizopo kwenye katiba na sheria ya uchaguzi za Daruso , “amesema Profesa Kimambo.

Amesema kutokana na maamuzi hayo uongozi wa chuo kwa kufuata hati idhini unaelekeza kuwa michakato yote inayohusiana na uchaguzi huo inapaswa kusitishwa kwa muda hadi hapo malalamiko hayo yatakapofanyiwa kazi.

“Wanafunzi wote anaombwa kuwa watulivu na kuepuka mambo au vitendo vyenye kupelekea uvunjifu wa amani, ”amesema Profesa huyo.

No comments

Powered by Blogger.