Full-Width Version (true/false)


Utata waibuka mazishi ya Bilago


 

Kigoma/Dar. Spika wa Bunge, Job Ndugai na baadhi ya wabunge wa CCM jana waliondoka nyumbani kwa aliyekuwa mbunge wa Buyungu (Chadema), Kasuku Bilago, Kakonko bila kushiriki mazishi muda mfupi baada ya kufikishwa mwili wa marehemu kutoka Dodoma.

Bilago alifariki dunia Mei 26 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alipokuwa akitibiwa. Mwanasiasa huyo anatarajiwa kuzikwa leo.

Kabla ya kuondoka, Spika Ndugai alitoa salamu za Bunge na pia zilitolewa salamu za Serikali huku akisema wamehuzunishwa na kifo hicho kwa vile mchango wa mbunge huyo ulikuwa bado unahitajika ndani na nje ya Bunge.

Hata hivyo, baada ya kumalizika kwa salamu na spika kuondoka, utata ulizuka baada ya katibu wa Chadema mkoani Kigoma, Shabani Madede kusema kiongozi huyo wa mhimili wa Bunge na wabunge wa CCM waliamua kuondoka kwa vile walitaka mazishi yafanyike jana, ilhali familia na Chadema wamepanga kufanya leo.

Akizungumza na Mwananchi, mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Kigoma, Daniel Nsazugwako alikiri kuwa ni kweli ulitokea utata hata hivyo akasisitiza kuwa yeye si msemaji.

“Mimi sijui nani amebaki, kila mmoja ilibidi achukue utaratibu wake. Lakini Katibu (wa Bunge, Steven) Kagaigai atakueleza vizuri,” alisema.

Nsazugwako ambaye pia ni mbunge wa Kasulu (CCM), alisema wabunge hao (wa CCM), katibu wa Bunge, Kagaigai na Spika Ndugai waliondoka saa tisa kurudi mkoani Dodoma.
“Nimesikitika sana sana kwa kifo cha Bilago lakini sina la kufanya, katibu atakueleza kwa upana suala hili,” alisema mbunge huyo.

Akizungumzia utata huo, mbunge wa Muhambwe (CCM), Atashasta Nditiye alisema ilibidi waondoke kabla ya mazishi kwa kuwa awali walitaarifiwa kuwa Bilago angezikwa jana, lakini wakaambiwa baadaye kuwa atazikwa leo.

“Tumesikitishwa kwa sababu taarifa ilikuwa Bilago ataagwa Jumanne, atasafirishwa Jumatano kuja Kakonko na kuzikwa leo (jana), lakini imebidi wabunge na spika turudi Dodoma kwa sababu ruhusa yetu ni ya leo tu na kesho tunatakiwa bungeni,” alisema.

Katibu wa Bunge, Kagaigai alipoulizwa kuhusu utata huo alisema, “Waulize waliopo huko, mimi sijui.”

Spika Ndugai alipopigiwa simu alitaka atumiwe ujumbe mfupi na hata alipotumiwa hakujibu mpaka gazeti hili likiwa linakwenda mtamboni.
Hata hivyo mbunge wa Momba, (Chadema), David Silinde alisema ulijitokeza utata kati ya Bunge na familia kuhusu siku ya kuzika. “Kwa sababu wao (Bunge) walishinikiza kuzika leo (jana) na familia ikitaka kuzika kesho (leo), baada ya kushindwa kuelewana wamezira na kuondoka,” alisema.

Mwili wa mbunge huyo uliwasili jana mjini Kigoma kwa ndege ya kukodi ukitokea Dodoma alikoagwa na wabunge, Jumanne.
     

No comments

Powered by Blogger.