Full-Width Version (true/false)


vyakula vimepanda bei mwezi huu wa Ramadhan

 

Mwezi mtukufu wa Ramadhan unaendelea. Ni mwezi ambao waumini wa dini ya Kiislamu wanalazimika kwa mujibu wa dini yao kufunga kujizuia kula na kunywa kuan-zia alfajiri hadi kuzama kwa jua.

Mwezi huu huandama kila mwaka na waumini wa dini ya Kiislamu nchini wanaungana na wenzao duniani kote kutekeleza ibada ya funga.
Swaumu ya Ramadhan kama ilivyo maarufu kwa waumini wa dini hiyo ni moja ya nguzo tano inayotekelezwa na waumini kwa minajili ya kuwajenga kuwa wacha Mungu.
Unaposoma makala haya ni vyema kutambua kuwa siku 29 au 30 ni za kheri na za kuchuma mema kama mafunzo ya dini ya Kiislam yanavyo-sisitiza.
Waislamu duniani kote wana-kumbushwa kushikamana vilivyo na mafunzo haya ili hatimaye iwe sababu ya wao kupata fadhila zinazotokana na kutekeleza ibada hii muhimu na adhimu.
Mbali na mwezi huu kuwa mwezi wa kuchuma mema bado unaingia dosari kila mwaka kutokana na utamaduni uliojengeka wa kupandisha bei za vyakula.
Kutokana na utamaduni huo, hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Maja-liwa aliwatoa hofu waumini wa dini ya Kiislam kwamba katika Ramadhan ya mwaka huu bei za vyakula hazitapanda huku akiwataka wakuu wa mikoa na wilaywa nchi kusimamia jambo hilo.
Kupanda kwa bei za vyakula kume-kuwa kukisababisha adha kwa wau-mini ambao hutumia bidhaa hizo kwa ajili ya futari.
Kwa baadhi ya wafanyabiashara pengine kwao ni fursa ya kujiingizia kipato zaidi lakini huacha maumivu na manung’uniko kwa watumiaji wa bidhaa hizo.
Wasemavyo wananchi
Mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam Mwanaisha Issa anashangazwa na upandishwaji wa bei za bidhaa mwezi huu wa Ramadhani huku akisema kuwa ni vyema wafanyabiashara wakaangalia upya bei za bidhaa.
Anasema hali hiyo inawaumiza wengi kwani bidhaa hizo ikiwemo nazi, maharage, ndizi, viazi na magimbi ni muhimu na lazima zitumike kwa waumini walio wengi. “Mimi huwa nashangaa kuona wafanyabiashara wanatumia nafasi hii ya muandamo wa mwezi wa Ramadhan kupandisha bei za bidhaa, mbaya zaidi hivi sasa mchele nao huenda ukawa pigo kwetu kwani bei nazo zinaweza kupanda,”anasema.
Mwanaisha anasema huu ni mwezi wa kusaidiana na kuonyesha upendo, hivyo ni vyema wafanyabiashara wakaonyesha upendo wao kwa kupunguza bei za bidhaa badala ya kupandisha.
“Tunahitaji pia kuwa na utulivu katika nafsi, lakini kwa kitendo hiki cha bidhaa kupanda bei kila Ramadhan si siri mioyo yetu haina utulivu,”anasema.
“Halafu ukiangalia hivyo vitu vinavyopandishwa bei ni muhimu sana kwa sababu futari bila mafuta au sukari bado haijakamilika, lakini pia kuna mchele ambao hutegemewa kwa daku,”anasema.
“Tutawezaje kumudu gharama hizo, tunaomba Mungu atufanyie wepesi wafanyabiashara washushe bei, wasiwe tayari kupandisha bei, bila hivyo hali itakuwa mbaya,” anasema.
Mwanaisha anaungwa mkono na Salim Ally wa Buguruni Malapa kwa kusema kwamba upandishaji wa bei za bidhaa limekuwa jambo la kawaida kila ifikapo mwezi huu.
“Kwa kweli tunashindwa kujua nini hasa chanzo cha tatizo hili, kila mwaka sisi ni watu wa kuumia katika mwezi wa Ramadhan, mbaya zaidi katika hali ya kawaida kabla ya mwezi huu bei za biadhaa zinakuwa za kawaida,”anasema.
Husna Ismail, mkazi wa Kariakoo anaiomba Serikali kuingilia kati suala hili ikiwezekana kuwachukulia hatua wanaopandisha bei kiholela. “Haiwezekani watu wanajiamulia tu kupandisha bei eti kwa sababu watumiaji ni wengi, hii si sawa hawa watu wasiruhusiwe kuuza kama wakibainika kupandisha bei kiholela,”anasema.
Akizungumzia upandishaji bei za bidhaa wakati wa mfungo wa Ramadhan, sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum anasema kuongeza bei za bidhaa si tu ni kupunguza riziki katika biashara bali hata kukosa thawabu.
“Wafanyabiashara hao ni vyema wakakumbuka lililobora zaidi kwa sababu anaweza kuona kuwa kupandisha bei ni faida lakini thawabu ndiyo bora zaidi,” anasema.
Amewaomba wafanyabiashara kuangalia namna ya kupunguza bei za bidhaa zao ili kuwarahisishia waumini kutekeleza ibada tukufu ya funga.
Kuhusu sukari na mafuta ameiomba Serikali kuangalia utaratibu mzuri ili kuhakikisha bidhaa hizo zinapatikana kwa urahisi kwa kuwa hutumika zaidi mwezi wa Ramadhan. “Kwa hili sina wasiwasi naamini Serikali yetu itajitahidi kuhakikisha bidhaa hizo ambazo kwa sasa zimekuwa na mapungufu zinapatikana,” anasema.
“Wito wangu kwa Waislamu ni kwamba Ramadhan imefika, hivyo tufunge kwa kuchunga mipaka yake, tuutumie mwezi huu kuomba zaidi ili tusamehewe makosa yetu na pia tufunge kwa kuliombea taifa letu,”anasema.
Wafanyabiashara
Mfanyabiashara wa magimbi katika soko la Buguruni Said Mohammed anasema kwamba kupanda kwa bidhaa kipindi cha mwezi wa Ramadhan ni suala ambalo hata wao wanaumizwa na hali hiyo.
Anasema kwamba kutokana na ushuru wanaotozwa wakati wa kusafirisha bidhaa hizo ndiyo hasa sababu ya wao kulazimika kupandisha bei bidhaa zao.
“Ushuru tunatozwa mkubwa, unakuta gunia moja tunatozwa Sh10,000, kwa hiyo na sisi tunauza kwa bei ambayo angalau inaweza kurudisha gharama japo si kwa sana,”anasema.
Hata hivyo mbali na kutozwa ushuru huo Mohammed pia amewaomba wafanyabiashara kuwa na moyo wa ubinaadamu kwani mwezi huu mbali na kuwa mtukufu lakini anaweza kukosa baraka ya biashara ya miezi inayofuata.
Pia anasema kwa sasa anauza fungu moja la magimbi kwa Sh1,000 hadi 2,000 mwaka jana aliuza kwa Sh1,000 hadi 1,500. “Hata hivyo bei hazikuongezeka sana, ukiangalia mwaka jana na mwaka huu kilichoongezeka ni Sh 500 pekee,” anasema.
Mfanyabiashara mwingine wa ndizi soko la Mabibo Fredy Masawe anasema bei za ndizi huwa hazitabiriki zinaweza kupanda au kushuka kila mwezi, inategemea na upatikanaji wake. “Mfano mwaka jana tuliuza ndizi kwa bei ya chini, hata hapa wanaona bei zimepanda lakini wakija tena mwezi Juni bei zikawa chini, hata sisi hatupendezewi na hii hali,” anasema Masawe.
Anasema wanauza fungu lenye ndizi nne kuanzia Sh1,000 bukoba, mshale wanauza ndizi saba kwa Sh1,000 mzuzu nne Sh1,500.
Kwa mujibu wa Masawe bei hazikupungua wala hazikuongezeka sana. “Kama si gharama za usafiri kupanda bei zingeshuka na kuwapa nafuu wafungaji.”
“Kwa hapa Mabibo wanacholalamikia sana ni nazi kwa sasa nazi unaipata kuanzia Sh600, 700 hadi 1,000 lakini cha kushangaza kabla ya mwezi huu nazi walikuwa wakiinunua hadi kwa Sh400 tena kubwa’’ anaongeza Masawe.
Anaishauri Serikali iangalie jinsi ya kudhibiti upandishwaji holela wa ushuru wa bidhaa kwani ndicho kinachochangia wananchi kuumia hasa mwezi huu.
“Cha kushangaza kila ifikapo mwezi huu lawama zinakuja kwetu, wengine wanadai kuwa bei zinapanda kwa sababu uhitaji ni mkubwa lakini ukweli ni kwamba sisi hatupendezewi na hii hali,” anasema.
“Japo mimi si miongoni mwa wanaofunga lakini nipo pamoja na ndugu zangu Waislam katika kuhakikisha wafanyabiashara tunawatendea haki, ifikie hatua mwezi huu uwe wa kuuza bidhaa kwa bei ambazo hazitoleta manung’uniko kwa wananchi,”anasema.
Viongozi wa soko
Katibu wa wauza ndizi katika soko la Temeke Stereo, Said Mzuzuri anasema kupanda kwa bei ya bidhaa mwezi huu wakulima wanahusika kwa asilimia kubwa.
Anasema kuna baadhi ya bidhaa mwezi huu zinakuwa na uhitaji mkubwa kwa hiyo mkulima anauza bei ya juu akijua lazima watu watanunua. “Kwa kipindi hiki wateja ni wengi, na bidhaa kama magimbi, ndizi na viazi zinatumika sana, kwa hiyo mkulima akiona watu kama ishirini wanakwenda kununua na yeye anaamua kuuza kwa bei anayoitaka,” anasema na kuongeza kuwa:
“Mkulima akiuza mfano kwa Sh2,000 mfanyabiashara akija huku anauza kwa Sh3,000 ili kuhakikisha anarejesha gharama aliyoitumia na kupata faida, hapa ndipo manung’uniko yanapoanzia,” anafafanua.
Mzuzuri amewaomba wakulima kuacha tabia ya kupandisha bei bidhaa kwani hali hiyo haiwatesi wafanyabiashara pekee bali hata Waislamu wanaotumia futari.
Hata hivyo anakiri kuna wafanyabiashara wenye tatizo na wanahitaji kudhibitiwa: “Kwa wafanyabiashara tutaangalia namna ya kuwadhibiti kwa kuwa wapo wanaopandisha kiholela kwa sababu tu ni mwezi wa Ramadhan, hawa tutawawajibisha,”anasema.
Mwenyekiti wa Soko la Ilala, Issa Malisa anasema sababu kubwa ya kupanda kwa bei za bidhaa ni gharama za usafiri kuwa juu.
“Tatizo madereva wanapenda kupandisha bei za kusafirisha mazao kutoka shamba kuja mjini, kwa hiyo utakuta mfanyabiashara anauza ili kufidia gharama zake za usafiri,” anaongeza.
     

No comments

Powered by Blogger.