Full-Width Version (true/false)


Wabunge Zanzibar walia na wasaniiWajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wameitaka serikali kuwainua wasanii wa Zanzibar hasa wa utamaduni na taarab asilia. 
Wakichangia bajeti ya Wizara ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa mwaka 2018/2019 katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, wamesema wengi wa wasanii hao wanaishi katika hali duni.

Wamefahamisha kuwa, wasanii hao wamefanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi kupitia sanaa zao, hivyo si vyema kuwaacha wakisumbuka na maisha huku kazi zao zikinufaisha wajanja wachache.

Mwakilishi wa Jimbo la Chakechake Suleiman Sarahan, amesema kuwa wasanii wa zamani wanakosa haki miliki ya kazi zao, na wale wa sasa hawapati manufaa kutokana na kazi zao.

Aidha, Suleiman ameitaka serikali kuwabana wasanii wanaoziimba tena nyimbo za wasanii wa zamani na kuangalia maslahi yao binafsi.

Naye, mwakilishi wa viti maalum wanu Hafidh Ameir, ametaka serikali kuvibana vyombo vya habari hasa redio na televisheni vinavyotumia nyimbo za wasanii bila ya kulipa mirabaha.

Ameir ameeleza kuwa, Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), linaongoza kwa kutolipa mirabaha hiyo, huku akidai shirika hilo linadaiwa zaidi ya shilingi milioni 80.

No comments

Powered by Blogger.