KATIKA kuhakikisha wanaongeza hamasa ya timu kuelekea mechi ya
pili ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, mabosi wa Yanga
walivamia mazoezi ya timu hiyo na kumwaga noti kwa wachezaji.
Yanga keshokutwa Jumatano inatarajiwa kuwakaribisha wapinzani wao
Rayon Sports ya Rwanda katika mchezo huo wa makundi utakaopigwa kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga tayari imepoteza mchezo wa kwanza katika kundi lao kwa kufungwa na USM Alger ya Algeria kwa kufungwa ugenini mabao 4-0.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, mabosi hao
walifika katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika juzi kwenye Uwanja wa
Chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam yakiongozwa na
Mkongoman, Zahera Mwinyi.
Mtoa taarifa huyo alisema mara baada ya kufika mazoezini, mabosi hao
walionekana kufuatilia kwa makini na baada ya kumalizika walipata nafasi
ya kuzungumza na viongozi, benchi na kikubwa kuwapa hamasa ya mchezo
ujao dhidi ya Rayon na badaye kila mchezaji na kiongozi wa benchi la
ufundi alipewa shilingi 50,000.
“Leo tulipata ugenini wa ghafla wa viongozi kutoka kamati ya mashindano
wakiongozwa na mwenyekiti wake Nyika (Hussein), Lukumayi (Samuel) na
kiongozi mmoja jina lake siri ambaye yeye ndiye aliyetoa fedha hizo.
“Fedha hizo zilitolewa baada ya mazoezi kumalizika na viongozi hao
kuzungumza machache, kikubwa wamesisitiza umuhimu wa mechi licha ya
timu kukabiliwa na matatizo ya kifedha,” alisema mtoa taarifa huyo.
Aidha, Championi Jumatatu lilimtafuta kocha Zahera kuzungumzia hilo,
akasema: “Ninafurahi kuona hamasa kubwa ikitolewa kwa wachezaji wangu
katika kuelekea mechi na Rayon.
“Kama nilivyokwambia awali, bado baadhi ya wachezaji wameonekana kuweka
mgomo kutokana na madai yao ya mishahara, lakini nafarijika kuwaona
wengine wakifika mazoezini.”
No comments