Full-Width Version (true/false)


Wanafunzi 165 wajazwa mimba Mpwapw


ZAIDI ya wanafunzi 165 wa shule za sekondari Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma, wameacha shule kutokana na kupata mimba kuanzia mwaka 2015 hadi Machi mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya hiyo, Lenard Msigwa wakati akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ulinzi wa wanawake na watoto katika mamlaka za serikali za mitaa kilichoandaliwa na Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF).

Msigwa alisema kuwa takwimu hizo, zimepatikana kutokana na kesi zilizoripotiwa, lakini hali ni mbaya zaidi kuliko inavyodhaniwa, kwa kuwa watoto wengi hawatoi taarifa pindi wanapoacha shule kwa ajili ya mimba na hivyo kudhaniwa kuwa wameacha shule kwa sababu za utoro.

"Kwa mfano kwa mwaka huu huu peke yake kuanzia mwezi Januari hadi Machi jumla ya wanafunzi 39 wameacha shule, kwa sababu ya mimba na hao ni wale tu ambao kesi zao zimeripotiwa, lakini tatizo ni kubwa kuliko picha tunayoiona, hivyo wadau wa elimu na serikali, bado ina kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa tunapambana hasa na mimba za utotoni," alisema Msigwa.

Alisema kwa mwaka 2015, wanafunzi 15 waliacha shule kutokana na mimba, mwaka 2016 wanafunzi 42 na mwaka 2017 wanafunzi 69. Kuanzia Januari hadi Machi mwaka 2018, wanafunzi 39 wameacha shule kwa kupata mimba.

Aidha alibainisha kuwa wakati mwingine wanapotaka kuchukua hatua dhidi ya wahusika, waliowapa mimba wanafunzi hao, wanakutana na changamoto kutoka kwa wazazi, ambao huitumia Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kumalizana na waliowapa mimba watoto wao.

"Sheria hii inamruhusu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 kuolewa kwa idhini ya wazazi," alisema Msigwa.

Akizungumza na wadau hao wa mtoto, Mkuu wa Operesheni kutoka CDF, Evance Rwamuhuru alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa kamati hiyo ni kumaliza tatizo la mimba za utotoni wilayani Mpwapwa, ambalo linakatisha masomo ya wanafunzi wengi wa kike na hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya wahusika.

Aliwataka wazazi na walezi wa watoto wanaokatishwa masomo yao, kwa kupata mimba kushirikiana na vyombo vya sheria ili wahusika waweze kukamatwa, kwani kwa kufanya hivyo, kutamaliza tatizo hilo.

Alisema mapambano ya kutokomeza mimba za utotoni, yanakuwa magumu kutokana na wazazi na walezi kutotoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria, badala yake huamua kumalizana na waliowapa mimba watoto wao na hivyo kuwapa kiburi wahusika.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa, Nuruprudensia Nassari alisema kuwa wengi wanaofikishwa mahakamani, kwa kesi za kuwapa wanafunzi mimba ni wale walioshitakiwa kwa makosa ya kubaka, ambapo ndani yake kuna kosa la kuwapa mimba wanafunzi.

"Hatuna kesi za kuwapa mimba wanafunzi, kesi nyingi zinazofunguliwa kwetu ni zile za ubakaji ambapo ndani yake sasa ndiyo kuna upatikanaji wa mimba," alisema Nassari.

Hata hivyo, alisema kuwa kuna baadhi ya watoto ambao wakifikishwa mahakamani, huwa wanatoa ushirikiano, lakini kuna baadhi ambao huwakataa wale waliowapa mimba, hata kama mzazi amemfikisha mahakamani mhusika.

No comments

Powered by Blogger.