Full-Width Version (true/false)


Wanaume ‘wanakimbia’ kupima Ukimwi


 

Dar es Salaam. Wakati Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (Pepfar) ukitoa takriban Sh1 trilioni kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya VVU nchini, wanaume wametakiwa kupima afya zao kwa hiari.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema idadi ya wanaume kujitokeza kupima maambukizi ya VVU ni ndogo ukilinganisha na wanawake.

Alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 15 ya ubia kati ya Marekani na Tanzania katika kupambana na Ukimwi.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Balozi wa Marekani nchini, Inmi Patterson na wadau mbalimbali wa afya.

Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2016/17, ulioangalia maambukizi mapya na kiwango cha kufubaza VVU, wanawake wanaongoza katika maambukizi mapya lakini ni wepesi kupima na kutumia dawa kikamilifu ikilinganishwa na wanaume.

“Ujumbe ni kuhakikisha Watanzania hasa wanaume wanajitokeza kupima VVU kujua hali zao, Ukimwi inaweza kuwa tatizo ila tatizo linaweza kuwa kutojua hali yako,” alisema.
Waziri Ummy alisema kupitia kampeni ya ‘Kupima na kutibu’ wamepanga kutembelea makundi yote na kuwashawishi wanaume kupima.

Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa, Watanzania milioni 1.4 wanaishi na VVU huku mikoa inayoongoza na asilimia yake kwenye mabano ikiwa ni Njombe (11.4), Iringa (11.3), Mbeya (9.3) na Mwanza kwa asilimia 7.2.

“Popote ambako tunajua tutawakuta wanaume wengi, sisi tutaweka kambi yetu pale, nawatoa hofu wanaume kwamba hatutalazimisha mtu kupima, lakini tukikukuta kwenye mpira, tamasha la muziki, tutakushauri upime” alisema Ummy.

Kuhusu kiwango cha fedha kilichotolewa na Pepfar, Ummy alisema kati ya Sh1 trilioni za kupambana na Ukimwi, Sh5.3 bilioni ni fedha za Serikali.

Katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alitoa agizo kwa wakuu wa mikoa nchini kuandaa mikakati itakayosaidia utekelezaji wa kampeni hiyo mpya ya ‘Pima na tibiwa’ kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijijini.

Majaliwa aliwaagiza viongozi hao wa mikoa na wilaya, kuanza kutekeleza kampeni hiyo katika maeneo yao.

“Wakuu wa mikoa waweke mikakati ili kuhakikisha kampeni hii inafika hadi vijijini, hususan wanaume wajitokeze katika kampeni hii,”alisema Majaliwa.

Kaimu Balozi Patterson alisema mpango huo umevuka lengo la utoaji huduma nchini.

“Kampeni mpya ya Pepfar15 itaendelea kwa mwaka wote wa 2018, ili kudhibiti janga hili ni muhimu kwa Watanzania wote waishio na VVU kupima na kujua hali za afya zao ili kuanza matibabu yatakayookoa maisha yao,” alisema Kaimu Balozi Patterson.

No comments

Powered by Blogger.