Full-Width Version (true/false)


Watu 30 kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho Muhimbili

Hospitali ya Taifa Mhimbili (MNH) leo tarehe 28-05-2018 imepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 200 vitakavyotumika kuhudumia wagonjwa wenye matatizo ya macho.


Msaada huo ambao unajumuisha kifaa maalum kinachotumika kupima uwezo wa kuona umetolewa na timu ya madaktari wa macho kutoka Japan ambao wamekuja MNH kwa ajili ya kambi maalum ya upasuaji wa macho.


Akikabidhi msaada huo Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaharu Yoshida amesema kwa muda  mrefu Japan imekua ikishirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili katika masuala mbalimbali hivyo ujio wa madaktari hao unazidi kuimarisha ushirikiano wao, lakini pia watalaam wa pande zote mbili wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji MNH, Dkt. Julieth Magandi ambaye amemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji Prof.  Lawrence Museru amesema Japan na Muhimbili wamekua na ushirikiano  takribani miaka 11 sasa na kwamba wamekuwa wakipeleka watalaam wao MNH kwa ajili ya kufanya upasuaji wa macho wa kibingwa.


“Napenda kutoa shukrani za pekee kwa Ubalozi wa Japan kwa ushirikiano tuliokua nao katika nyanja tofauti, wenzetu wamekua wakileta watalaam hapa na tumekua tukifanya nao kazi na kuzidi kujengeana uwezo,” amesema Dkt. Magandi.


Kuhusu kambi ya upasuaji wa macho amesema kambi hiyo ya siku tatu  ambayo imeanza leo jumla ya wagonjwa 30 wenye tatizo la mtoto wa jicho watafanyiwa upasuaji.


Naye Daktari Bingwa wa upasuaji macho Neema Kanyaro amesema katika Kliniki ya macho Muhimbili wataalam huona wagonjwa 15 hadi 20 kwa siku ambao wanatatizo la mtoto wa jicho.


Amesema tatizo hilo ni kubwa hususani kwa watu wazima na lina chukua nafasi ya kwanza katika matatizo ya macho yanayosababisha upofu kwa asilimia kubwa. Hata hivyo tatizo hilo linatibika kwa asilimia 100.

No comments

Powered by Blogger.