Full-Width Version (true/false)


WAZIRI MAHIGA AZINDUA RASMI OFISI ZA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI ISRAEL.Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amezindua rasmi ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Israel, katika jiji la Tel Aviv, siku ya jana tarehe 08 Mei 2018.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Israel, imesema kuwa uzinduzi huo ulihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Ayelet Shaked, Mabalozi wa nchi za Afrika na Watanzania wanaoishi nchini humo. Dkt. Mahiga akisalimiana na Waziri wa Sheria wa Israel, Bi. Shaked

Katika uzinduzi huo Dkt. Mahiga alitoa hotuba yake ambayo iliitaja Israel kama nchi ya kupigiwa mfano kwa sababu licha ya changamoto za kimahusiano na baadhi ya jirani zake lakini bado nchi hiyo imepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo cha umwagiliaji, viwanda, matibabu, TEHAMA, ulinzi na usalama, uhifadhi wa maji na masuala ya nishati ikiwemo nishati ya kutumia joto ardhi. Mhe. Shaked akiwahutubia watu walioudhuria hafla ya ufunguzi wa ofisi za ubalozi wa Tanzania

Akiongelea masuala ya ulinzi na usalama katika hotuba yake, Dkt. Mahiga alisema Watanzania hawataisahau Israel kwa kuwa ndiyo nchi iliyoisaidia Tanzania kuanzisha Jeshi la Kujenga Taifa ambalo mafanikio na mchango wa jeshi hilo unajulikana na kila Mtanzania.

Dkt. Mahiga pia aliishukuru nchi ya Israel kufuatia mawaziri wake wawili kufanya ziara za kikazi nchini Tanzania hivi karibuni, ambapo amewataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Ulinzi, Mhe. Avigdor Liberman aliyetembelea Tanzania tarehe 20 hadi 22 Machi 2018, na Waziri wa Sheria, Mhe. Ayelet Shaked ambaye alikuwa nchini tarehe 23 na 24 Aprili 2018. Dkt. Mahiga akiongea kwenye hafla hiyo.

Akiongea kwa niaba ya serikali ya Israel, Waziri wa Sheria wa nchi hiyo, Mhe. Shaked alibainisha kuwa nchi yake ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo kusaidia teknolojia ya kisasa kwenye kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji. Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Job Masima akiwahutubia watu walioudhuria hafla hiyo.

Naye Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Job Masima alishukuru wadau wote ikiwemo serikali ya Israel kwa kumpa ushirikiano wa kutosha uliofanikisha upatikanaji wa ofisi hiyo na kufunguliwa rasmi hiyo jana tarehe 08 Mei 2018, huku akiwahakikishia umma uliohudhuria hafla hiyo na wadau wengine kuwa wasisite kufika kwenye ofisi hiyo kwa ajili ya kupata huduma watakazozihitaji. Dkt. Mahiga akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watanzania waishio Israel

Kwa kuhitimisha hafla hiyo, Dkt.Mahiga aliwakaribisha Waisrael kuja Tanzania kwa ajili ya kufanya utalii kwa kuwa Tanzania ina vivutio lukuki vya utalii. Alisema zaidi ya watalii elf 50 huja Tanzania kila mwaka, lakini hawatoshi kutokana na wingi wa vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

No comments

Powered by Blogger.