Full-Width Version (true/false)


Waziri Masauni atoa agizo hili kwa Jeshi la Polisi Mkoani Iringa


NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni,  ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani Iringa kujipanga kuhakikisha ajali za barabarani zinatokomezwa.

Masauni alisema  hayo juzi mkoani hapa alipofanya ziara ya kushtukiza eneo la kizuizi cha magari cha Igumbilo, Manispaa ya Iringa.

Katika ziara hiyo, Masauni alisema lengo la kufanya hivyo lilikuwa kuangalia kama magari yanayofanya safari za masafa marefu yanakuwa na madereva wawili na si mmoja.

Alisema  ajali zimepungua kwa asilimia 37.7 kwa nchi nzima lakini kwa mkoa wa Iringa zimeongezeka jambo ambalo limemfanya kuchunguza nini chanzo cha ongezeko hilo.

“Nchi nzima ajali zimepungua kwa asilimia 37.7 lakini kwa mkoa wa Iringa naona hawajatusaidia kwenye tatizo hili. Nimetafakari,  nimejiuliza na wenzetu wa jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani, nikaona bora nije hapa nione tatizo nini ili niweze kulishughulikia,”alisema.

“Tumegundua kwamba magari yanayofanya safari za masafa marefu wengine wanaondoka na madereva wawili lakini wakiwa njiani mmoja anashuka na kumwacha dereva mmoja jambo ambalo akifika mwisho wa safari pengine anakuwa amechoka sana.”

Katika hatua nyingine , mchakato wa kuhamisha na kujenga gereza jipya la mkoa wa Iringa utakaogharimu Sh. bilioni 12.2 umeshaanza.

Uhamishaji wa gereza hilo lililoko katika manispaa ya Iringa, unalenga kupisha nafasi kwa ajili ya upanuzi wa hospitali ya rufani ya mkoa  ambayo iko karibu na gereza hilo.

Akizungumza mjini hapa wakati wa hafla ya uzinduzi wa bodi mpya ya Parole, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa, Kamishina Msaidizi Mwandamizi Afwilile Mwakijungu, alisema gereza hilo litajengwa Mlowa, umbali wa kilomita saba kutoka lilipo gereza la zamani.

Hata hivyo, Mwakijungu alisema  ukosefu wa fedha ni changamoto inayokwamisha ujenzi kuanza kwa wakati.

No comments

Powered by Blogger.