Waziri Mkuu kuzindua kampeni ya upimaji VVU kuwahamasisha wanaume
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mwezi ujao, atazindua kampeni
maalum ya upimaji wa virusi vya UKIMWI (VVU) ambayo imelenga
kuwahamasisha wanaume wapime afya zao na kutambua hali zao.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akizindua maadhimisho ya miaka 15 tangu
kuanzishwa kwa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na
Kudhibiti Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (PEPFAR) kwenye ukumbi wa
Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
“Serikali tumeandaa kampeni maalum ya kuhamasisha upimaji wa VVU na
kuanza matumizi ya dawa za kufubaza VVU mara moja (Test and Treat), hasa
kwa wanaume. Kampeni hii itazinduliwa rasmi na mimi mwenyewe jijini
Dodoma tarehe 19 Juni 2018,” amesema Waziri Mkuu.
“Takwimu zinaonyesha watu ambao wako tayari kupima kwa hiyari yao
siku zote ni wanawake. Akinababa wakiambiwa hutoa sababu mara hiki, mara
kile. Nitoe wito kwa wanaume wote, tubadilike! Ni vema tushiriki
kampeni ya wanaume kujitambua na kupima ili tujue hali zetu,” amesema
aliongeza.
Aidha amewataka wadau wote wanaohusika na masuala ya UKIMWI washiriki
kikamilifu katika kampeni hiyo baada ya uzinduzi, na pia akawataka
Wakuu wa Mikoa mikoa yote nchini wasimamie kampeni hizo muhimu katika
mikoa yao hadi ngazi ya vijiji.
Amesema kuna mikoa 14 ambayo kiwango cha maambukizi kiko juu ya
wastani wa kitaifa wa asilimia 4.7 na akaitaja mikoa hiyo kuwa ni Njombe
wenye asilimia 11.4, Iringa (asilimia 11.3), Mbeya (asilimia 9.3),
Mwanza (asilimia 7.2), Kagera (asilimia 6.5) na Katavi (asilimia 5.9).
Mikoa mingine ni Shinyanga (asilimia 5.9), Songwe (asilimia 5.8) Ruvuma
(asilimia 5.6) Pwani (asilimia 5.5) Tabora (asilimia 5.1) pamoja na
Tanga, Dodoma na Geita ambayo yote ina asilimia 5.0 ya maambukizi.
Waziri Mkuu ameitaja mikoa mingine sita ambayo ina ongezeko kubwa la
watu wanaoishi na VVU kuwa ni Iringa (asilimia 11.3), Mwanza (asilimia
7.2), Kagera (asilimia 6.5), Tanga (asilimia 5.0), Dodoma (asilimia 5.0)
na Manyara (asilimia 2.3).
Akimkaribisha, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Bi. Ummy Mwalimu alisema Tanzania kwa sasa ina watu karibu
milioni moja ambao wako kwenye matibabu ya kufubaza VVU.
No comments