Full-Width Version (true/false)


Waziri wa mambo ya nje wa China akutana na Kiongozi wa korea kaskazini


China imesema waziri wake wa mambo ya nje amekutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un mjini Pyongyang, ikiwa ishara ya kuboreka kwa mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Katika tangazo la wizara ya mambo ya nje, imeelezwa kuwa waziri huyo Wang Yi amemhakikishia Kim Jong Un kwamba China itaiunga mkono kikamilifu Korea Kaskazini katika kuukarabati uchumi wake baada ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa, ambavyo vilisimamisha asilimia 90 ya biashara kati ya nchi hizo.

Kim alifanya ziara mjini Beijing mwezi Machi, iliyofuatiwa na mlolongo wa juhudi za kidiplomasia, ukiwemo mkutano baina ya Kim na rais wa Korea Kusini Moon Jae-In wiki iliyopita, na mwingine baina ya Kim na Rais Donald Trump wa Marekani unaotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.

Wachambuzi wanaamini vikwazo vya China ndivyo vilivyoilazimisha Korea Kaskazini kuunga mkono juhudi hizo za kidiplomasia.

No comments

Powered by Blogger.