Full-Width Version (true/false)


Wizara ya Mambo ya Nje kutekeleza sera ya Rais Magufuli


Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wametakiwa kufanya kazi kwa weledi ili kutimiza malengo ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Kauli hiyo ilitolewa leo jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Waziri Mahiga alieleza kuwa Wizara inatakiwa kuweka Sera na mikakati ya utekelezaji kwa kuzingatia miongozo na maelekezo ya Viongozi wa juu akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. “Sera ya Serikali ya awamu ya tano ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, hivyo Sera yetu ya Mambo ya Nje lazima ijikite katika diplomasia ya uchumi wa viwanda”. Dkt. Mahiga alieleza.

Dkt. Mahiga alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka watumishi kuhakikisha kuwa Wizara inatekeleza majukumu yake kwa kujiwekea ratiba ya kuyakamilisha kwa kuzingatia hotuba za Mhe. Rais Magufuli alizozitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kikao cha Mabalozi na Mhe. Rais Magufuli na kikao cha watumishi wa Wizara na Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Wizara yake imejipanga ipasavyo kuhakikisha kwamba jukumu la kuchochea uchumi wa nchi kupitia Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika diplomasia ya uchumi inatekelezwa kikamilifu.

Prof. Mkenda alisema Wizara kwa kushirikiana na ofisi zake za Ubalozi, licha ya changamoto mbalimbali inazokutana nazo, lakini imekuwa ikitafuta fursa za uwekezaji, mitaji, masoko, utalii na elimu na kuzileta nchini ili kufikia azma ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020.

No comments

Powered by Blogger.