Abiria wapanda bure mabasi ya mwendokasi

Leo imekuwa ni asubuhi njema kwa abiria wa mabasi
yaendayo haraka (Udart), baada ya kupanda usafiri huo bure.
Abiria wa mabasi hayo, wamejikuta wakipanda bure kutokana na
kudaiwa kuwepo kwa hitilafu katika mfumo wa tiketi.
Madirisha ya vyumba vinavyotumika kukatia tiketi yalikuwa
yamefungwa huku mabasi yakiendelea kubeba abiria kama kawaida.
Abiria wengi walionekana kufurahia kusafiri bure, hata hivyo baadhi ya
wanaotumia kadi wamejikuta wakilipia usafiri huo kwa kuwa
wanatumia mashine maalum za kugonga.
"Kumbe ni bure, sikujua inaniuma kama nikadai vile,"amesema abiria
mmoja baada ya kugonga kadi yake.
Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, ofisa mawasiliano wa Udart, Deus
Buganywa amesema atatoa taarifa kwa vyombo vya habari baadaye.
Abiria mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Daudi Joshua amesema
kupanda usafiri bure kumemfurahisha kwa kuwa anaona ni fidia ya
usumbufu wa kusubiri magari hayo kwa muda mrefu.
"Huduma ya usafiri huu haitabiriki, tumekuwa tukipata usumbufu
mkubwa, sasa leo sijui wanatoa ofa kusafisha makosa yao," amesema
Joshua, mkazi wa Luguruni Mbezi.
Mwandishi wetu alishuhudia wafanyakazi wa Udart wakiwa wamesimama
vikundi wakijadiliana.
Tangu jana asubuhi, huduma za usafiri huo ziliendelea bila wananchi
kukata tiketi.
No comments