Full-Width Version (true/false)


Alipwa mara 10 ya mshahara wa JPM

 

KAMATI Maalum ya Uchunguzi wa gesi iliyoundwa na Spika Job Ndugai, mwishoni mwa mwaka jana,imewasilisha ripoti yake jana na katika mambo iliyobaini ni mmoja wa watumishi wa Kampuni ya PanAfrican Energy kulipwa mshahara wa Sh. milioni 96, ambao ni mara 10 ya mshahara wa Rais John Magufuli ambao ni Sh. milioni 9.5 kwa mwezi. 

Novemba 17, mwaka jana, Spika Ndugai aliunda kamati maalum mbili ikiwamo hiyo ya kuchunguza na kuishauri serikali kuhusu sekta ndogo ya gesi baada ya ripoti mbalimbali zilizowasilishwa bungeni kuonyesha Tanzania hainufaiki ipasavyo na rasilimali hiyo. 

Akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo kwenye Viwanja vya Bunge jijini Dodoma jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dunstan Kitandula, mbali na mambo mengine, alisema kamati yake ilibaini wabia wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), katika miradi ya gesi wamekuwa wakilinyonya shirika hilo kimgawo kwa kuonyesha hesabu zao kuwa wana gharama kubwa za uendeshaji.

Alisema miongoni mwa mbinu zinazotumika ni mishahara ya wafanyakazi wa kigeni kuwa mikubwa kulinganishwa na mishahara ya watumishi wazawa kwenye kampuni hizo. 

"Kwa mfano, tulibaini katika kampuni ya PAET watumishi wa kigeni wanalipwa mishahara mikubwa kulinganishwa na watumishi wa wazawa. 

Kuna mtumishi yumo ndani ya menejimenti ya kampuni analipwa mshahara wa Sh. milioni 96 kwa mwezi ambao ni mara nne ya mshahara wa watumishi wa kitanzania," alisema. 

Taarifa za kuwapo kwa kigogo huyo anayelipwa mshahara mkubwa kipindi hiki ambacho Rais Magufuli ameshaagiza kiwango kikubwa cha mshahara kiishie Sh. milioni 15, ilionekana gumzo miongoni mwa watu waliohudhuria hafla ya uwasilishwaji wa ripoti hiyo. 

Kitandula ambaye pia ni Mbunge wa Mkinga (CCM), hakutaja jina la kigogo huyo wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya kamati yake, hata hivyo. 

Pia alisema kwenye mkataba wa TPDC na PAET, kuna kipengele kinachoiruhusu kampuni hiyo kufanya malipo bila idhini ya TPDC pamoja na kujirejeshea kodi na gharama za ada za watoto na matumizi ya nyumbani kwa vigogo wa kampuni hiyo. 

"TPDC ndiyo ina majukumu ya kufanya ukaguzi kwa mwekezaji na hadi sasa Sh. bilioni 183 hazijapatiwa ufumbuzi, hivyo kuikosesha TPDC gawio la Sh. bilioni 79," alisema. 

Kitandula ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, alisema hali hiyo imesababisha hasara kwa serikali ya Sh. bilioni 291 ambayo ni sawa na bajeti ya wizara nne kwa mwaka ujao wa fedha ambazo ni pamoja na Wizara ya Kilimo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Viwanda.

No comments

Powered by Blogger.