Full-Width Version (true/false)


Aslay Afunguka Penzi Lake na Nandy

Aslay Afunguka Penzi Lake na Nandy
NI kijana wa Temeke, alianza kufahamika mwaka 2011 baada ya kutoa ngoma iitwayo Nakusema, alitamba pia akiwa chini ya Band ya Yamoto Band iliyoanzishwa mwaka 2013 lakini baada ya bendi hiyo kufa mwaka 2017, alianza kufanya muziki akiwa solo.

Ana umri wa miaka 23, ana mashabiki kibao ndani na nje ya Bongo, mwezi Januari mtandao namba moja Afrika wa kusambaza nyimbo ‘online’ uitwao Not Just Ok, kutoka Nigeria ulimtaja kuwa mwanamuziki wa Bongo Fleva anayefanya vizuri zaidi nchini humo!

Nakupa zaidi; Ndani ya mwezi mmoja huachia ngoma mbili mpaka tatu, ngoma yake inayotamba kwa sasa inaitwa Nibebe, video zake nyingi hupendelea kufanyia uswazi au vijijini na anatengeneza ‘chemistry’ nzuri akikaa kwenye wimbo na mwanamuziki Nandy!

Hapo vipi? Bila shaka umenusa chochote kwa kijana huyu ambaye msikilizaji wa Muziki wa Bongo Fleva huwezi kuepuka kumsikia kutokana na fujo alizonazo za kuachia ngoma. Jina lake la kuzaliwa anaitwa Aslay Isihaka Nassoro a.k.a Dogo Aslay na kazi zake za muziki zinasimamiwa na meneja wake wa muda mrefu aitwaye Chambuso.

Dogo Aslay, hivi karibuni ameingia kwenye ‘headlines’ baada ya kuposti kwenye mitandao ya kijamii mjengo wa maana ambao wengi walijiongeza kwamba ni mjengo wake. Lakini pia mkali huyu wa ngoma ya Subalkheri Mpenzi, mara kwa mara amekuwa akiingia kwenye headlines kwa mambo mengi ikiwemo ‘life style’ yake. Kufahamu mengi kuhusu yeye huyu hapa akifanya mahojiano na Showbiz Xtra;

Showbiz Xtra: Kwanza nini siri ya video zako nyingi kufanyia uswazi na vijijini?

Aslay: Unajua mimi nimezaliwa uswazi na nimekulia uswazi. Kwa hiyo mara nyingi nimekuwa nikihitaji kuwakilisha asili yangu. Lakini ukweli ni kwamba nyuma ya hilo baada ya kutoka Yamoto, kwangu kidogo maisha yaliyumba, nikawa sina uwezo wa kufanya video nje ya nchi kama Sauz, ila niliamini sauti yangu inaweza kunibeba, na nilipotoa kazi zilipokelewa vizuri. Kwa hiyo uswazi ni mahali sahihi zaidi kwangu.

Showbiz Xtra: Kwa hiyo huna mpango kabisa wa kutoka zaidi ya hapo kufanya video?

Aslay: Mipango ipo, mwaka huu ni mwaka wa maajabu, watu wategemee makubwa kwa maana mbali na uswazi tutakwenda huko ambako mashabiki wetu wanapenda kuona pia tunafanya kazi.

Showbiz Xtra: Mtandao wa Not Just Ok, ulikutaja kuwa unasikilizwa zaidi Afrika Magharibi na ukaahidi kufanya kazi na wewe, mipango ipo vipi?

Aslay: Mipango ipo chini ya menejimenti yangu wao ndiyo wanaweza kuizungumzia zaidi.

Showbiz Xtra: Hapo awali umezun-gumzia baada ya kutoka Yamoto Band maisha yaliyumba, tofauti zaidi ni ipi kipindi upo na Yamoto na sasa ukiwa solo?

Aslay: Hakuna tofauti zaidi, labda kipato kule nilikuwa ninapata kipato kidogo sasa napata zaidi lakini maisha ni yaleyale.

Showbiz Xtra: Kuhusu kipato unatajwa kuwa miongoni mwa wanamuziki wenye mkwanja mrefu kwa sasa, ikiwa ni pamoja na kuishi ‘luxury life’, tuweke wazi una mkwanja kiasi gani benki na mali gani hasa unamiliki?

Aslay: Mungu anajaalia kwa kiasi chake, lakini siwezi kuweka wazi juu ya pesa ninazomiliki wala mali, lakini maisha ninayamudu kwa kupitia kipaji changu.

Showbiz Xtra: Mjengo uliyoposti hivi karibuni ni wako na upo maeneo gani?

Aslay: Kuna mipango mingi sana mwaka huu nitaiweka wazi kwenye kikao na waandishi wa habari wote, hata hili tutalizungumzia hapo.

Showbiz Xtra: Lakini mashabiki zako wangependa kufahamu kwa sasa, weka wazi hata kidogo?

Aslay: Wawe wavumilivu kila kitu kitakuwa wazi.

Showbiz Xtra: Vipi kuhusu nyumba uliyopewa kipindi kile na uongozi wa Yamoto Band, bado unaimiliki au nini kinaendelea kwenye nyumba hiyo?

Aslay: Tuzungumzie zaidi kazi yangu ya muziki.

Showbiz Xtra: Unahusishwa kutoka na wanawake wanaokuzidi umri, umewahi kuhusishwa kuwa na uhusiano na Vick Kamata, hili lina ukweli kiasi gani?

Aslay: Halina ukweli wowote.

Showbiz Xtra: Lakini pia unahusishwa kutoka kimapenzi na Nandy, hili je unalizungumziaje?

Aslay: Nandy ninafanya naye kazi tu sina uhusiano naye.

Showbiz Xtra: Malizia kwa lolote.

Aslay: Yaah! Mashabiki wangu wategemee mambo makubwa, kuna picha nimeposti mtandaoni za mwanamke anayeonekana mjamzito ni projekti yangu mpya, vitu vingi vinakuja mwaka huu.

No comments

Powered by Blogger.