Full-Width Version (true/false)


Baada ya wapinzani kuitwa 'Mbwa' Mwenyekiti wa Bunge aomba radhi

 

Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga amewaomba radhi wabunge wa upinzani kwa tafrani iliyoibuka juzi na kusababisha aondolewe kitini, akisema hakumsikia mbunge akitamka neno “mbwa”. Amesema kama angemsikia mbunge wa Jang’ombe (CCM), Ally Omary ‘King’ akitamka neno hilo, angechukua hatua. 

Alisema tayari ameshawaomba radhi wabunge wa upinzani kwa kilichotokea bungeni juzi. Mzozo uliibuka bungeni baada ya King kusema: “Nasikia milio ya mbwa. Kama tutawatoa itakuwa vizuri.” Alisema hayo wakati wabunge wa upinzani wakipiga kelele, baadhi wakitaka kutoa taarifa baada ya awali kusema, “ukisikia majuha wanapongezana, usidhani wamefanya la maana”. 

Juhudi za Giga kutuliza kelele za kuomba kutoa taarifa na kumtaka afute kauli yake zilishindikana na muda mfupi baadaye akashtukia Spika Job Ndugai amesimama pembeni yake akimsubiri asimame ili achukue uongozi wa kikao hicho, jambo lililoshangiliwa na wabunge wa upinzani

Lakini jana, Giga alisema hakumsikia King akitamka maneno hayo wakati wa mjadala wa hotuba ya Wizara ya Fedha na Mipango juzi. 

Akizungumza na Mwananchi jana katika viwanja vya Bunge, Giga alisema hakusikia maneno aliyotoa King, lakini alipoondoka katika kiti cha Spika alitambua kuwa mbunge huyo alitoa maneno hayo. “Mwanzo nilisikia majuha na kwa kuwa kelele na zomeazomea zilikuwa nyingi sikusikia. Kwa kuwa ni kipindi cha Ramadhani, mathalan ningesikia ningemtaka mbunge yule (King) ayafute lakini kwa kuwa sikuyasikia nilishindwa,” alisema. 

Alisema King alimweleza kuwa hakuwaita mbwa, bali alifananisha milio ile na ya mbwa. “Nilimweleza (King) kusema vile tafsiri ya maneno yale ni walewale wabunge kwani yako wazi, lakini alipokuja Spika na mimi kushuka chini nilipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wabunge wa upinzani na niliwataka radhi,” alisema. 

Hisia tofauti Tukio hilo limepokewa kwa hisia tofauti. Kaimu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Abdallah Mtolea alisema Spika alitumia busara kutuliza mzozo. Mtolea ambaye ni mbunge wa Temeke (CUF), alisema Giga anapaswa kujifunza kwa kilichotokea. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema Giga alisababisha kikao kuyumba. 

“Sidhani kama busara ilitumika Spika kuja kuchukua uongozi,” alisema. “Mwenyekiti angeweza kusimamia Bunge hata kwa dakika tano.” Ally Saleh (Malindi-CUF), alisema alichokifanya King hakikupaswa kwa kuwa alitoa lugha ya kuudhi ambayo kikanuni haitakiwi na kwamba Spika angeacha hali hiyo, Bunge lisingekalika. Alisema si kwamba Giga ni kiongozi mbaya, “kwa kuwa kuna kipindi hata refa mzuri huzidiwa na mchezo

Lakini, Mussa Simba (Singida Mjini - CCM), alisema Giga alishindwa kumudu Bunge na ndio maana kitendo cha Spika kuingia, kilirejesha utulivu. 

Naye John Heche (Tarime Vijijini- Chadema) alisema jambo hilo si la kawaida na halifurahishi. 

“Yote yalisababishwa na lugha iliyotolewa na King kutokuwa ya kibunge,” alisema. Wabunge wa CCM, Mendard Kigola (Mufindi Kusini) na Seif Gulamali (Manonga) walisema kelele ndiyo chanzo ingawa lugha iliyotumiwa na King haikuwa sahihi. Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Anatropia Theonest alisema kinachotakiwa ni kiti cha Spika kusimamia haki.

No comments

Powered by Blogger.