Full-Width Version (true/false)


Bili ya umeme yakwamisha taa za barabarani

 

WAKALA wa Barabara (Tanroads) mkoa wa Arusha, umesema unahitaji Sh. milioni 11.2 kila mwezi kwa ajili ya uendeshaji wa taa za barabara kuanzia Sakina hadi Tengeru. 

Hayo yalisemwa na Meneja wa Tanroad Mkoa wa Arusha, Mhandisi John Kalupale, alipozungumza na Nipashe katika mahojiano maalum. Watumiaji wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 14.1 wamekuwa wakishangaa kutowashwa kwa taa hizo nyakati za usiku na wakati mwingine hata taa za kuongozea mgari eneo la Mianzini huwa haziwaki. 

Mhandisi Kalupale alisema ili taa hizo ziwake wakati wote wa usiku, wanatakiwa kulipa bili ya umeme kwa Tanesco ya Sh. milioni 11.2 kila mwezi. 

Alisema bajeti kwa ajili ya taa za kuongozea magari na za barabarani haikuwa imetengwa wakati wa ujenzi wa barabara hiyo. Hata hivyo, alisema sasa hivi wamepewa maelekezo kutoka makao makuu ya Tanroads kuandika makadirio ya gharama za uendeshaji wa mradi huo.

 “Tayari tumeshafanya makadirio hayo na kupata gharama halisi, kipande cha barabara ya SakinaTengeru tunahitaji Sh. milioni 11.2 kila mwezi na sehemu ya barabara ya Sakina-Ngaramtoni tunahitaji Sh. milioni 6.04 kwa mwezi. “Kutokana na fedha tulizokuwa nazo kuwa chache, ilikuwa vigumu kuendeleza miradi hii kwa sababu tungeiingiza serikali katika madeni na Tanesco kama tungekuwa tunawasha taa hizo,” alisema. 

Alisema kwa mfano, taa zilizowekwa sehemu ya barabara ya Arusha-Namanga baada ya kukamilika kwake ziliwaka kwa muda wa miezi 10 tu, lakini zikazimwa kutokana na kukosa fedha. 

Wakizungumzia kushindwa kuwashwa kwa taa hizo, baadhi ya wakazi jijini hapa walishauri kurekebishwa kwa mfumo wa taa hizo ili utumie umeme wa jua. 

Amina Mollel na Yasin Abdallah, walisema kutokuwaka kwa taa za kuongezea magari kwa kipindi kirefu kunaleta shida kwa watembea kwa miguu kuvuka barabara kwa urahisi. 

“Nyakati za jioni tunapotaka kuvuka barabara tunashindwa kwa sababu magari hayasimami kutokana na kutokuwaka kwa taa za kuongozea magari,” alisema Amina. 

“Tatizo limejitokeza kwa wanafunzi wanapotoka shule, lazima wazazi tukawasubiri kwenye vivuko ili kuwavusha barabara kutokana na hali halisi ya barabara yetu,” alisema Abdalah. 

Akizungumzia maeneo ya barabara yaliyoharibika kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Arusha, Mhandisi Kalupale, alisema kampuni iliyokuwa ikijenga barabara hiyo itayafanyia ukarabati. 

Aidha alisema wanakabiliwa na changamoto nyingine ya uharibifu wa miundombinu ya barabara hiyo kutokana na ujenzi wa miradi ya maji ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha (Auwsa), inayoendelea kutekelezwa pembezoni mwa barabara hiyo.

No comments

Powered by Blogger.