Full-Width Version (true/false)


Hamisa Mobetto, mama yake wajibu mapigo vijembe vya familia ya Diamond

 
Hatimaye vile vijembe vinavyorushwa na familia ya mwanamuziki Diamond Platinumz vikidaiwa kumlenga mwanamitindo Hamisa Mobetto, upande wa pili umeanza kujibu mapigo. 

Jana Juni 1, 2018 baada ya mwanamuziki Diamond Platinumz kutoa wimbo Iyena, mama yake, dada na baadhi ya wanafamilia wa lebo ya WCB waliandika maneno ambayo mashabiki walitafsiri kama ni ujumbe kwenda kwa wazazi wenzake, Hamisa Mobetto na Zari Hassan. 

Familia hiyo ilikuwa ikimsifu Zari aliyetangaza kuachana na Diamond, Februari 14, 2018 kwa madai ya kudhalilishwa, kuwa ni mwanamke msafi na anayefaa kuwa mke wa mwanamuziki huyo. 

Pamoja na Zari kusifiwa, familia hiyo ilionyesha nia ya kutaka kuwapatanisha huku dada wa Diamond, Esma akidai kuwa kaka yake amepauka tangu aachane na mwanamke huyo, kwa kuwa aliyenaye sasa hajui kupika wala kufanya usafi wa nyumba. 

Vijembe hivyo imeonekana kumchefua mama mzazi wa Mobetto ambaye ameamua kufunguka kumtetea mwanaye. 

"My baby.....endelea kuwa strong (imara) mwanangu, hakuna binadamu yeyote anayeweza shusha hadhi yako wala kukudhalilisha, sana sana wanajidhalilisha wenyewe.” 

MCL Digital leo ilimtafuta mama Mobetto ili afafanue kauli hiyo na pia kuthibitisha kama kweli ina uhusiano na kinachoendelea katika mitandao ya kijamii. 

"Ni kweli niliamua kukaa kimya na nitaendelea kukaa kimya, nimeandika hivyo ili watu wajue Hamisa ana mzazi wake yuko hai na sio mtoto aliyekosa wazazi hadi ifikie hatua ya kumweka midomoni kila kukicha.” 

Naye Hamisa aliamua kujitetea kwa kutoa maoni katika posti ya Diamond iliyopo katika mtandao wa Instagram akisema ayamalize na ndugu zake akidai kuwa wamekuwa wakimwandama. 

“Wewe ni mwanaume ongea na ndugu zako, oa mwanamke wanayemtaka na pia mimi ninafanya haya yote ili mtoto wetu akikua asiyaone haya lakini ndugu zako hawabebeki,” ameandika.

No comments

Powered by Blogger.