Full-Width Version (true/false)


Homa ya Bonde la Ufa yaua watu watano


 Watu watano wamefariki dunia kutokana na mlipuko wa Homa ya Bonde la Ufa nchini Kenya wiki iliyopita ikiwa ni muongo mmoja umepita tangu ugonjwa huo uliposababisha vifo vya watu zaidi ya 200 nchini humo. 
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huo hatari unasambazwa kwa binadamu na mbu au kwa kugusa mizoga ya wanyama, damu au viungo vyao.

Afisa wa Kamati ya Afya wa Kaunti ya Wajir, Kaskazini Mashariki mwa Kenya, Abdihakim Billow, ambako vifo hivyo vimetokea amesema watu wawili walifariki hospitali huku wengine watatu wakifia nyumbani, ambapo watu wengine wawili wanaoshukiwa kuugua ugonjwa huo wamelazwa hospitali.

Hatua kadhaa za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku uuzaji wa nyama ya ng'ombe kwa siku 10.

Maafisa wanakadiria kwamba tangu kuanza kwa mwezi huu, mifugo 50 imekufa, mlipuko wa Homa ya Bonde la Ufa kwa mara ya mwisho ulitokea Kenya Novemba mwaka 2006 hadi Machi 2007 na kugharimu maisha ya watu 234.

No comments

Powered by Blogger.